Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeendelea kutoa Elimu ya Usalama wa Usafiri Majini kwa wakazi na wadau wa fukwe ya Kilambo, mkoani Mtwara, tarehe 10 Februari 2026. Hatua hii ni sehemu ya jitihada za kuimarisha usalama na uelewa katika shughuli za usafiri na usafirishaji majini nchini.
Elimu hii imeelekezwa hasa kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri majini, waendesha vyombo, wavuvi, na wasafiri, ikilenga kuwajengea uwezo wa kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu za usalama ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
Washiriki pia wameelimishwa juu ya matumizi sahihi ya vifaa vya usalama, ikiwemo jaketi okozi, kufanya ukaguzi wa vyombo kabla ya safari, na kuzingatia taarifa za hali ya hewa kabla ya kuanza safari yoyote majini.
Maafisa wa TASAC wamekumbusha wadau kwamba uzingatiaji wa sheria na kanuni za usafiri majini si chaguo bali wajibu, na kutokuzingatia masharti haya kunaweza kusababisha madhara makubwa, ikiwemo kupoteza maisha na mali.
Kwa upande wao, wakazi na wadau wa fukwe ya Kilambo wamepongeza TASAC kwa kuendelea kuwafikia na kuwapatia elimu muhimu, wakisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza usalama, kuimarisha shughuli zao za kiuchumi, na kulinda maisha ya watumiaji wa usafiri majini.
Elimu hii ya Usalama, Ulinzi, na Utunzaji wa Mazingira Majini mkoani Mtwara ilianza tarehe 9 Februari 2026 na itaendelea hadi tarehe 13 Februari 2026, ikitarajiwa kufikia wakazi wengi zaidi katika eneo hilo.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni