Breaking


Jumanne, 17 Februari 2026

TRC YAANZA RASMI USAFIRISHAJI WA MIZIGO KWA KUTUMIA CONTAINER CARRIERS SGR

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanza rasmi usafirishaji wa makasha kwa kutumia reli ya Standard Gauge, hatua inayolenga kupanua wigo wa biashara, kupunguza msongamano wa mizigo bandarini na kurahisisha usafirishaji wa mizigo kwenda mikoa ya kati ya nchi.

Akizungumza wakati wa kuanza safari ya treni ya kwanza ya makasha kutoka Pugu kuelekea Ihumwa mkoani Dodoma, Kaimu Mkurugenzi wa Usafirishaji wa TRC, Focus Makoye Sahani, amesema treni hiyo inasafiri umbali wa takribani kilometa 420 kutoka Dar es Salaam. 

Amesema hatua hiyo ni mwanzo wa usafirishaji wa makasha baada ya TRC kuanza kusafirisha abiria pamoja na mizigo mbalimbali ikiwemo kichele kuanzia mwezi Julai, pamoja na saruji inayopakiwa Pugu. 

Kwa mujibu wa Sahani, TRC imeanza upakiaji wa makasha katika eneo la Pugu, huku ikifanya maboresho ya miundombinu ikiwemo Malindi Yard karibu na eneo la Gerezani  ili kuimarisha shughuli za upakiaji wa makasha. 

Hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa mizigo bandarini, sambamba na utekelezaji wa maelekezo ya Mkurugenzi Mkuu ya kuhakikisha uwepo wa Vituo vya Kontena vya Ndani (ICD) katika Morogoro, na Ihumwa . 

Ameongeza kuwa safari ya kuelekea Morogoro huchukua muda mfupi, huku mzigo unaoelekea Dodoma ukishushwa katika ICD ya Ihumwa, ambako kuna eneo kubwa na miundombinu ya kutosha kuhudumia makasha. 

Akitoa wito kwa wafanyabiashara, Sahani amewahimiza Watanzania kutumia usafiri wa reli ili kupunguza utegemezi wa malori kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, akisisitiza kuwa huduma ya reli ya Standard Gauge ni rahisi, salama na yenye ufanisi. 

Hii ni mara ya kwanza kwa TRC kutumia container carries,  toka ilipoanza usafirishaji wa  mizigo kwa SGR Juni 27, 2025.

Hakuna maoni: