Vikwazo vitano visivyo vya kikodi kati ya 10 vilivyokuwa vikisababisha msongamano wa malori na usumbufu kwa wafanyabiashara na wasafirishaji katika mpaka wa Tunduma na Nakonde, zimepatiwa ufumbuzi kupitia juhudi za pamoja za serikali za Tanzania na Zambia.
Hatua hiyo inatajwa kuwa chachu ya kuimarisha biashara za kimataifa katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha ujirani mwema kilichofanyika mpakani Tunduma na kuwakutanisha Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka pande mbili, wakiongozwa na Balozi Mahmoud Thabit Kombo, na Mulambo Haimbe wa Zambia.
Akizungumza baada ya kikao, Waziri Kombo, amesema moja ya mafanikio ni kuridhia kwa serikali ya Zambia kuanza kutoa huduma kwa saa 24 kama ilivyo katika utaratibu wa Kituo cha Pamoja.
Hatua hii itapunguza ucheleweshaji wa mizigo na msongamano wa magari ya mizigo katika eneo la mpakani.
Aidha, pande hizo mbili zimekubaliana kusomanisha mifumo ya forodha ya TANCIS inayotumika Tanzania na ASYCUDA Plus inayotumika Zambia, ili kuwezesha ubadilishanaji wa taarifa haraka na kuongeza uwazi katika shughuli za mpakani.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni