Kwa mujibu wa NBC News, video hiyo yenye urefu wa takribani dakika moja, ilikuwa ikihusisha madai ya udanganyifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Hata hivyo, sehemu ya mwisho ya video hiyo ilizua hasira kubwa baada ya kuonyesha nyuso za Barack na Michelle Obama zikiwa zimepachikwa juu ya vichwa vya sokwe, huku wimbo maarufu wa “The Lion Sleeps Tonight” ukisikika kwa nyuma.
Akizungumza na waandishi wa habari usiku wa kuamkia Ijumaa, Trump alikana kuunga mkono ubaguzi wa rangi lakini akaweka wazi msimamo wake kuhusu kuomba radhi.
“Bila shaka nakataa sehemu za ubaguzi wa rangi zilizomo kwenye video hiyo, lakini sina mpango wa kuomba msamaha,” alisema Trump.
Awali, Ikulu ya Marekani ilijaribu kujitetea kwa kueleza kuwa video hiyo ilikuwa ni sehemu ya vichekesho vya mtandaoni (meme) vilivyosambaa kwenye mitandao ya kijamii. Hata hivyo, baada ya kukumbwa na ukosoaji mkali kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu na baadhi ya wanasiasa, wakiwemo wanachama wa chama chake mwenyewe, hatua ilichukuliwa kuiondoa video hiyo.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani alisema kuwa tukio hilo lilitokana na kosa la kibinadamu.
“Mfanyakazi mmoja wa Ikulu aliichapisha video hiyo kwa bahati mbaya. Tayari imefutwa,” alisema msemaji huyo.
Hadi sasa, Trump hajatoa ufafanuzi wa moja kwa moja kuhusu ni mfanyakazi gani aliyehusika na tukio hilo wala kama hatua zozote za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni