Breaking


Alhamisi, 5 Machi 2026

JKCI YAENDESHA KAMBI YA UCHUNGUZI WA MAGONJWA YA MOYO KWA WAUMINI KKKT MBEZI BEACH

 


Waumini 93 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania-KKKT, Usharika wa Mbezi Beach, jijini Dar es salaam, wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali yakiwemo ya Moyo.

Hii ni katika jitihada za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kupunguza vifo vya ghafla vinavyosababishwa na kutofanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.

Uchunguzi huo ulifanyika kupitia kambi maalumu iliyoendeshwa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete-JKCI, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania-KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Usharika wa Mbezi Beach.

Kambi hiyo ni sehemu ya mkakati wa JKCI wa kuimarisha kinga na kutoa elimu dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza hususan magonjwa ya moyo, shinikizo la juu la damu na kisukari.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha zoezi hilo, Afisa Masoko wa JKCI, Agness Mndasha, amesema jitihada hizo zinaungwa mkono na maboresho makubwa ya sekta ya afya yanayofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, jambo linaloiwezesha JKCI kupanua wigo wa huduma za kibingwa na kuokoa maisha ya Watanzania wengi zaidi.

Bendriba Lyanga muumini wa Kanisa hilo ameipongeza JKCI kwa kuwafikia wananchi moja kwa moja, huku akisema amekutana na madaktari bingwa wa moyo na kufanyiwa vipimo na kupata ushauri kitu kilichomfungua macho na kumpa matumaini mapya.


Hakuna maoni: