Breaking


Ijumaa, 13 Machi 2026

KANYE WEST AAMRIWA KULIPA FIDIA YA DOLA 140,000 KWA FUNDI BAADA YA MGOGORO WA MALIPO


Mahakama ya jiji la Los Angeles nchini Marekani imemuamuru rapa maarufu Kanye West, anayejulikana pia kwa jina la Ye, kulipa fidia ya dola 140,000 (takribani shilingi milioni 365.4 za Kitanzania) kwa fundi aliyemfungulia kesi akidai hakulipwa stahiki zake wakati wa ukarabati wa nyumba ya msanii huyo iliyopo Malibu.

Fundi huyo, anayejulikana kwa jina la Tony Saxon, alidai kuwa hakulipwa ipasavyo kwa kazi aliyofanya katika jumba la ufukweni la West na pia alifukuzwa kazi kwa njia isiyo halali. Katika kesi hiyo, Saxon alikuwa akiomba fidia ya dola milioni 1.7 (takribani shilingi bilioni 4.4), lakini jopo la majaji (jury) lilimpa dola 140,000 pekee kama fidia.

Kesi hiyo ilisikilizwa katika Mahakama ya Los Angeles Superior Court, ambapo ushahidi uliwasilishwa kutoka kwa Kanye West pamoja na mke wake Bianca Censori kuhusu mchakato wa ukarabati wa nyumba hiyo ya kifahari.

Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, Saxon aliwasilisha kesi hiyo mwaka 2023 akidai kulikuwa na mazingira hatarishi ya kazi, kutolipwa mishahara yake pamoja na kufukuzwa kazi bila sababu za msingi. Aidha, alidai kupata majeraha ya shingo na mgongo alipokuwa akifanya kazi katika mradi huo na kuomba fidia ya matibabu.

Saxon alieleza kuwa West alimwahidi kumlipa dola 20,000 kwa wiki, lakini alidai alipokea malipo mara moja tu ya dola 20,000 pamoja na dola 100,000 ambazo zilitajwa kuwa ni kwa ajili ya gharama za ujenzi.


Hata hivyo, timu ya mawakili wa Kanye West ilipinga madai hayo ikidai kuwa Saxon hakuwa mkandarasi mwenye leseni halali na kwamba aliharibu muundo wa nyumba hiyo wakati wa kazi ya ukarabati. Pia walipinga madai ya majeraha aliyodai kuyapata kwa kuwasilisha video inayomuonesha Saxon akitumbuiza na bendi na kujiviringisha sakafuni, wakisema hali hiyo inaonyesha kuwa hakuwa na majeraha makubwa kama alivyodai.

Katika ushahidi wake mahakamani, Kanye West alisema hakumbuki kwa undani matukio mengi yaliyotajwa na Saxon, ingawa alikiri kuwahi kulalamika kuhusu harufu ya mfanyakazi huyo wakati wa kipindi cha kazi.

Uamuzi huo wa mahakama umehitimisha mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya pande hizo mbili kuhusu malipo na mazingira ya kazi katika mradi wa ukarabati wa nyumba ya rapa huyo.


Hakuna maoni: