Breaking


Alhamisi, 19 Machi 2026

KWAHANI FC YATWAA UBINGWA MASAUNI CUP


Timu ya Kwahani FC imetwaa ubingwa wa michuano ya Masauni Cup baada ya kuichapa Mwembeladu FC kwa mikwaju ya penalti 1-0, kufuatia sare ya bao 1-1 ndani ya muda wa kawaida. Ushindi huo umeifanya Kwahani FC kujinyakulia kombe pamoja na kitita cha shilingi milioni tano.

Katika mchezo huo wa fainali, Kwahani FC walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Abdalla Himidi, kabla ya Mwembeladu FC kusawazisha kupitia kwa Tariq Mzee katika dakika za mwisho za mchezo, hali iliyosababisha timu hizo kwenda kwenye mikwaju ya penalti.

Penalti ya ushindi iliyofungwa na Mundhir Omar Hassan ndiyo iliyoihakikishia Kwahani FC ubingwa huo. Kwahani FC ilitinga fainali baada ya kuichapa Kwalinatu FC mabao 2-1 katika hatua ya nusu fainali, huku Mwembeladu FC ikiingia fainali kwa ushindi wa penalti 3-1 dhidi ya Kiswandui. Mwembeladu FC imeondoka na zawadi ya shilingi milioni mbili.

Akizungumza katika hafla ya kufunga mashindano hayo, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe Juma, amesema wizara itaendelea kushirikiana na wadau wa soka ili kuhakikisha malengo ya Serikali ya kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana yanafikiwa, pamoja na kuwapatia fursa za ajira ndani na nje ya Zanzibar.

Amesema Serikali ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ina dhamira ya dhati ya kuifanya sekta ya soka kuwa chombo cha kuwawezesha vijana kiuchumi na kuwasaidia kujenga mustakabali wao.

Aidha, Waziri huyo amesisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuona vijana wanatumia vipaji vyao kujitangaza kimataifa, akimtaja mchezaji Feisal Salum kama mfano wa mafanikio kwa vijana wanaocheza soka.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema mashindano hayo yameanzishwa kwa lengo la kuwapa vijana fursa ya kuonesha vipaji vyao na kuimarisha mshikamano kupitia michezo.

Aidha, amewataka vijana kushiriki mashindano hayo kwa nidhamu, kuheshimu sheria za mchezo na kudumisha mshikamano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Hakuna maoni: