Serikali imetangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati, ikizialika kampuni na wawekezaji wa kimataifa kuchangamkia nafasi hizo ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Felchesmi Mramba, ametoa kauli hiyo katika kikao maalum cha India–Africa Partnership kilichofanyika wakati wa mkutano wa Bharat Electricity 2026 unaoendelea nchini India.
Mhandisi Mramba amesema Tanzania ina mazingira rafiki ya uwekezaji na inaendelea kujipambanua kama moja ya maeneo yenye fursa kubwa katika sekta ya nishati barani Afrika.
Fursa hizo zinapatikana katika maeneo mbalimbali ikiwemo miradi ya kuzalisha umeme, kusafirisha na kusambaza umeme, pamoja na uwekezaji katika nishati jadidifu kama jua, upepo, jotoardhi na umeme wa maji.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mramba, uwezo wa uzalishaji umeme nchini umefikia takribani megawati 4,500 na unatarajiwa kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.
Hivyo, amesisitiza kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na wadau wa kimataifa katika kuendeleza miradi ya kimkakati kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi-PPP, akiwahakikishia wawekezaji uwepo wa mazingira wezeshi, sera thabiti na dhamira ya dhati ya Serikali katika kusimamia na kutekeleza miradi ya nishati.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni