Breaking


Jumatatu, 6 Aprili 2026

MASAUNI AWATAKA VIJANA KULINDA MISINGI YA MUUNGANO


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amewataka wanafunzi wa elimu ya juu na vijana nchini kuendelea kulinda na kutetea misingi ya Muungano iliyoasisiwa na waasisi wa Taifa.

Ameyasema hayo Aprili 06, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la kumuenzi Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar.

Masauni amesema Sheikh Karume ameacha historia ya kudumu kutokana na mchango wake mkubwa katika kuunganisha Watanzania na kutetea maslahi ya wananchi wanyonge.

Amesema kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa kiongozi huyo, hususan juhudi zake za kuasisi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.

Aidha, amemtaja Karume kuwa kiongozi imara aliyesimamia maendeleo ya kijamii na kiuchumi Zanzibar ambayo yameendelea kudumishwa hadi leo.

Masauni ameongeza kuwa sera zake zilizoigusa jamii, ikiwemo elimu bure, matibabu bure na makazi ya kisasa, zitabaki kuwa kumbukumbu muhimu kwa Taifa.

Pia alisisitiza kuwa Karume alikuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha umoja wa Afrika na ndoto ya Shirikisho la Afrika.

Kwa upande wake, Dkt. Richard Muyungi amesema kongamano hilo la kwanza Tanzania Bara linalenga kuhamasisha vijana kutambua mchango wa waasisi wa Muungano.

Hakuna maoni: