Breaking


Jumanne, 17 Machi 2026

MAJIKO YA UMEME YALETA MAPINDUZI SHULE SITA ZA MSINGI TABORA


SHULE sita za msingi Manispaa ya Tabora, zikiwemo za wanafunzi wenye mahitaji maalum (viziwi na wasioona), zimejengewa majiko ya kisasa yanayotumia umeme kwa ajili ya kupikia chakula cha wanafunzi kupitia mradi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi shuleni.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa mradi huo kutoka Wizara ya Nishati, Deo Alex, wakati wa ziara ya ukaguzi iliyowahusisha wataalamu kutoka Wizara hiyo pamoja na Shirika la Chakula Duniani (WFP) katika Manispaa ya Tabora, mkoani Tabora.

Amesema mradi huo unafadhiliwa na wadau wa maendeleo, wakiwemo Serikali ya Uingereza (UK FCDO), na unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya WFP na Shirika la Sustainable Energy for All (SEforALL).

Kwa mujibu wa Alex, utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya kutekeleza agizo la Serikali linalozitaka taasisi zote zinazohudumia chakula kwa watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi ya kupikia.

Aidha, amewataka watekelezaji wa mradi huo kuhakikisha wanazingatia viwango vilivyowekwa pamoja na kuukamilisha kwa wakati ili kuanza kutoa manufaa yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Afisa Elimu Maalum na Mratibu wa Afya Shuleni wa Manispaa ya Tabora, Feliciana Muyaga, amesema kukamilika kwa majiko hayo kutaondoa changamoto ya wapishi kupika nje, hususan wakati wa mvua.

Ameongeza kuwa mradi huo utarahisisha shughuli za upishi mashuleni na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma ya chakula.

Mazingira yatakuwa safi muda wote na afya ya wapishi pamoja na wanafunzi italindwa,” amesema Muyaga.

Pia amesema mradi huo utaongeza hamasa kwa wazazi kuchangia gharama za chakula mashuleni pamoja na kupunguza ukataji wa miti, hivyo kusaidia kulinda mazingira.

Ametaja Shule hizo kuwa ni Uhuru, Magereza, Furaha, Bombamzinga, Kizigo na Tabora Viziwi.

Naye, Meneja wa Mradi kutoka WFP Tanzania, Dkt. Geoffrey Ndegwa, amesema uamuzi wa kutumia majiko ya umeme umetokana na upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini, unaozalishwa kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo Mradi wa Julius Nyerere.

Amewasisitiza walimu kusimamia vyema miundombinu ya mradi huo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kuwanufaisha wanafunzi.

Amesisitiza shirika hilo linaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kufikia asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.

Hakuna maoni: