Breaking


Jumatano, 25 Machi 2026

WAZIRI NA MBUNGE WA ISIMANI, WILIAM LUKUVI AFARIKI DUNIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametangaza kwa masikitiko makubwa kifo cha aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Vangimembe Lukuvi, kilichotokea leo Machi 25, 2026, majira ya saa moja asubuhi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa alipokuwa akipatiwa matibabu kufuatia mshtuko wa moyo. Kifo chake kimeacha pengo kubwa katika uongozi na utumishi wa umma nchini kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi.

Katika salamu zake za rambirambi, Rais Samia ametoa pole kwa Spika wa Bunge, familia ya marehemu, wananchi wa Jimbo la Isimani pamoja na Watanzania wote walioguswa na msiba huo mzito. Amesisitiza kuwa marehemu Lukuvi atakumbukwa kwa uzalendo, uadilifu na juhudi zake katika kutumikia wananchi, akiwahudumia kwa moyo wa kujituma katika nyadhifa mbalimbali za uongozi serikalini.


Aidha, Serikali imesema itaendelea kutoa taarifa zaidi kuhusu taratibu za mazishi ya kiongozi huyo, huku ikiwataka Watanzania kuungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Kifo cha Mheshimiwa Lukuvi ni pigo kubwa si tu kwa wananchi wa Isimani bali pia kwa taifa kwa ujumla, lililompoteza kiongozi mwenye uzoefu na mchango mkubwa katika maendeleo ya kisiasa na kijamii nchini.

 

Hakuna maoni: