Mshambuliaji nyota wa Liverpool FC, Mohamed Salah, ametangaza rasmi kuwa ataondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu, akihitimisha safari yake iliyodumu kwa mafanikio makubwa ndani ya timu hiyo ya Ligi Kuu England.
Salah, mwenye umri wa miaka 33 na raia wa Misri, alijiunga na Liverpool mwezi Juni mwaka 2017 akitokea AS Roma, na tangu wakati huo amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi katika kikosi hicho, akichangia mafanikio mbalimbali ikiwemo mataji ya ndani na kimataifa.
Kupitia video aliyochapisha kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, Salah alithibitisha uamuzi huo huku akionesha hisia za huzuni na shukrani kwa mashabiki na klabu kwa ujumla.
“Kwa bahati mbaya siku hii imefika. Hii ni sehemu ya kwanza ya salamu zangu za kuaga,” alisema Salah katika ujumbe wake.
“Nitaondoka Liverpool mwishoni mwa msimu,” aliongeza, kauli iliyozua hisia miongoni mwa mashabiki wa soka duniani, hususan wapenzi wa Liverpool ambao wamekuwa wakimthamini kwa mchango wake mkubwa ndani ya klabu hiyo.
Kuondoka kwa Salah kunatarajiwa kuacha pengo kubwa ndani ya kikosi cha Liverpool, huku hatma ya nyota huyo ikisubiriwa kwa hamu kujulikana atatua klabu gani msimu ujao.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni