Serikali ipo mbioni kuanzisha mpango maalum wa Mageuzi ya Kijani utakaolenga kukijanisha Tanzania pamoja na kusafisha mazingira, ambapo programu zake zitatekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini kama sehemu ya juhudi za kuhifadhi na kulinda mazingira.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Yussuf Masauni, ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza Machi 13, 2026. Amesisitiza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kulinda mazingira, huku Serikali ikiendelea kuwapongeza wale wanaozingatia sheria za uhifadhi wa mazingira na kuwachukulia hatua kali wanaokiuka sheria hizo.
Amesema mpango huo umejikita katika maeneo mbalimbali ikiwemo upandaji miti kwa wingi ili kupunguza hatari ya kuenea kwa jangwa, uanzishaji wa bustani, usafishaji wa miji, pamoja na ulinzi wa vyanzo vya maji. Alieleza kuwa hatua hizo zitachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha afya za wananchi kwa kupunguza magonjwa yanayosababishwa na mazingira machafu.
Aidha, Waziri Masauni amewataka wawekezaji na Watanzania kwa ujumla kuhakikisha wanazingatia sheria na kanuni za uhifadhi wa mazingira katika shughuli zao za kila siku. Amesisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu au taasisi yoyote itakayobainika kuharibu mazingira.
“Tunawajibu wa kulinda mazingira. Ili yawe mazuri ni lazima sisi wenyewe tuyahifadhi, na ili yawe mabaya ni lazima sisi tuyaharibu. Serikali itaendelea kuhakikisha Watanzania wanatunza mazingira yao, na haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaoharibu mazingira kwa namna moja au nyingine,” alisema Masauni.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amesema ofisi yake inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha mazingira yanatunzwa licha ya changamoto kadhaa, ikiwemo udhibiti wa kelele chafuzi zinazotokana na baadhi ya kumbi za starehe.
Aidha, Mtanda ameiomba Ofisi ya Makamu wa Rais kuendelea kuimarisha juhudi za kuondoa gugumaji katika Ziwa Victoria ili kulinda samaki na ikolojia ya mazalia ya viumbe wa majini. Amesema shughuli za uvuvi ni mhimili muhimu wa uchumi kwa wananchi wa mkoa huo.
Ameongeza kuwa takribani asilimia 53 ya eneo la Mkoa wa Mwanza limezungukwa na maji, jambo linalohitaji uangalizi maalum katika uhifadhi wa mazingira, hususan vyanzo vya maji na mwambao wa Ziwa Victoria ili kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinaendelea kudumu.
Katika hatua nyingine, Waziri Masauni pia alitembelea maeneo yaliyoathirika na mafuriko yaliyotokea hivi karibuni mkoani Mwanza, yaliyosababisha uharibifu wa miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, nyumba pamoja na mali za wananchi.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni