Kumekuwa na sintofahamu nzito kwenye tasnia ya burudani nchini Nigeria baada ya chama cha ma-DJ kinachojulikana kama Nigerian DJ Association kutangaza marufuku ya ghafla kwa ma-DJ wote kupiga nyimbo za staa wa Afrobeats Burna Boy. Hatua hiyo imewashangaza mashabiki wengi wa muziki huo duniani, hasa ikizingatiwa kuwa Burna Boy ni miongoni mwa wasanii wanaotamba kwa hits kali zinazotikisa vilabu na majukwaa makubwa kimataifa.
Chanzo cha mvutano huo kinadaiwa kuwa ni tukio la ugomvi lililosambaa mitandaoni likimhusisha Burna Boy na DJ maarufu DJ Tunez, jambo lililoibua mjadala mkali miongoni mwa wadau wa burudani. Video hiyo imezua hisia tofauti kwa mashabiki, baadhi wakimtetea msanii huyo huku wengine wakitaka heshima zaidi kati ya wasanii na ma-DJ, ambao ni sehemu muhimu ya kusambaza muziki wao.
Katika taarifa yao, Nigerian DJ Association wameeleza kuwa kwa sasa nyimbo zote za Burna Boy zimeondolewa kwenye playlist za wanachama wao hadi uchunguzi utakapokamilika. Wakati hali ikiendelea kuwa tete, mashabiki wanasubiri kwa hamu kuona kama mgogoro huu utaisha kwa maridhiano au utazidi kuchochea mvutano ndani ya tasnia ya muziki wa Afrobeats.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni