Breaking


Jumanne, 10 Machi 2026

MWANAMKE ALIYEFYATUA RISASI NYUMBANI KWA RIHANNA ADAIWA KUCHAPISHA UJUMBE WA AJABU KABLA YA TUKIO


Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Ivanna Lisette Ortiz (35) anayekabiliwa na mashitaka ya kufyatua risasi katika nyumba ya msanii maarufu wa kimataifa Rihanna, anadaiwa kuwa alichapisha ujumbe wa ajabu kwenye mitandao ya kijamii wiki chache kabla ya tukio hilo kutokea.


Kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi, chapisho la Facebook lililowekwa Februari 23 kutoka kwenye akaunti inayodaiwa kuwa ya Ortiz lilikuwa na maneno ya kutatanisha yaliyomlenga moja kwa moja Rihanna. Katika ujumbe huo, Ortiz alionekana kujaribu kuwasiliana na mwimbaji huyo kwa maneno yasiyoeleweka, akidai kuwa alikuwa akingojea majibu yake badala ya “kujificha na kuzungumza naye kwa njia zisizo za moja kwa moja”.


Mbali na hilo, Ortiz pia anadaiwa kushiriki video nyingine ya kushangaza ambapo alimhusisha rapa mashuhuri Cardi B. Katika video hiyo, inadaiwa Ortiz alijirekodi akizungumza mbele ya kioo akiwa amevaa wigi na kaptura yenye rangi za bendera ya Marekani, huku akitoa kauli za kujisifu na kumtaja Cardi B akisema kuwa hawezi “kucheza naye”.


Taarifa za polisi zinaeleza kuwa tukio la kufyatua risasi lilitokea katika nyumba ya Rihanna iliyopo Los Angeles siku ya Jumapili. Wakati risasi kadhaa zilipigwa kuelekea nyumba hiyo, Rihanna aliripotiwa kuwapo ndani ya makazi yake, hata hivyo hakuna mtu aliyeripotiwa kujeruhiwa.


Maafisa wa usalama bado wanaendelea na uchunguzi kubaini sababu halisi ya tukio hilo, kwani hadi sasa nia ya mshukiwa haijathibitishwa rasmi.


Ortiz kwa sasa amefunguliwa mashitaka ya jaribio la kuua, huku mahakama ikiweka dhamana yake katika kiwango cha dola 10,225,000 za Marekani, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 26 za Kitanzania. Kesi hiyo inaendelea kufuatiliwa na mamlaka husika huku uchunguzi ukiendelea.

 

Hakuna maoni: