Breaking


Jumanne, 24 Machi 2026

NEMC YAJA NA MKAKATI WA “TAKA SIFURI” KUHAMASISHA WANANCHI KUONA TAKA KAMA FURSA YA KIUCHUMI


Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Taka, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira limejipanga kuhamasisha jamii kubadili mtazamo kuhusu taka na kuanza kuziona kama fursa ya kiuchumi badala ya uchafu. Kupitia maadhimisho hayo yatakayofanyika jijini Dar es Salaam, wananchi wanatarajiwa kupata elimu na uelewa mpana juu ya namna bora ya kusimamia taka kwa njia endelevu, ikiwa ni pamoja na kuzigeuza kuwa rasilimali zenye thamani na chanzo cha kipato.

Akizungumza na waandishi wa habari Mapema hii leo  Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria wa NEMC, Hamadi Taimuri Kisiwa, amesema maadhimisho hayo yatafanyika kuanzia Machi 28 hadi 30, 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja. Amesema tukio hilo litawakutanisha wadau mbalimbali wa mazingira, wajasiriamali pamoja na wananchi kwa ujumla ili kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu usimamizi endelevu wa taka.


Aidha, Kisiwa ameeleza kuwa kaulimbiu ya kimataifa kwa mwaka huu ni “Wezesha taka sifuri kwenye sekta ya chakula”, huku kaulimbiu ya kitaifa ikiwa ni “Taka ni Fursa”. Amesisitiza kuwa ujumbe huo unalenga kuibua fikra mpya kwa jamii kuona taka kama chanzo cha ajira na kipato badala ya uchafu. Ameongeza kuwa mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni.


Kwa mujibu wa Kisiwa, maadhimisho hayo pia yatajikita katika kuhamasisha matumizi ya dhana ya 3Rs ambayo ni Kupunguza (Reduce), Kutumia tena (Reuse) na Kurejeleza (Recycle). Hatua hii inalenga kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali zilizopo na kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira. Amesisitiza kuwa elimu hiyo ni muhimu katika kujenga jamii inayojali mazingira na kutumia rasilimali kwa njia endelevu.


Vilevile, matumizi ya mbinu hizo yanatarajiwa kupunguza kiwango cha taka kinachotupwa ovyo katika maeneo ya makazi na biashara, jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira pamoja na hatari za kiafya. Kupitia ubunifu wa kurejeleza taka, wananchi wanaweza kuzalisha bidhaa mbalimbali kama samani, mbolea na hata vifaa vya ujenzi, hivyo kuongeza thamani ya taka na kuchochea shughuli za kiuchumi.


Kwa ujumla, NEMC inaamini kuwa maadhimisho hayo yatakuwa chachu ya mabadiliko ya mtazamo kwa jamii, kutoka kuona taka kama tatizo hadi kuiona kama fursa ya maendeleo. Hatua hiyo inatarajiwa kuchangia si tu katika kulinda mazingira bali pia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kupitia ajira na ubunifu unaotokana na usimamizi sahihi wa taka.

Hakuna maoni: