Polisi wa jiji la Los Angeles nchini Marekani wameanza uchunguzi wa kina kufuatia tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa nyumba ya msanii maarufu wa muziki Rihanna iliyopo eneo la kifahari la Beverly Hills.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani, tukio hilo lilitokea Jumapili majira ya saa 7 mchana kwa saa za huko, ambapo mtu anayeshukiwa kuhusika na tukio hilo alifyatua takribani risasi kumi akiwa ndani ya gari lililokuwa limeegeshwa upande wa pili wa barabara karibu na jumba hilo.
Maafisa wa polisi wamesema kuwa moja ya risasi hizo ilipenya ukuta wa nyumba hiyo, ambayo mwimbaji huyo anaishi pamoja na mwenzi wake, rapa A$AP Rocky, pamoja na watoto wao. Hata hivyo, polisi wamethibitisha kuwa Rihanna alikuwa ndani ya nyumba wakati wa tukio hilo lakini hakupata majeraha yoyote.
Hadi sasa, msanii huyo bado hajatoa tamko rasmi kuhusu tukio hilo ambalo limeibua taharuki kubwa miongoni mwa mashabiki wake na wakazi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa za polisi, mshukiwa wa tukio hilo anadaiwa kuwa mwanamke mwenye umri wa takribani miaka 30. Inadaiwa kuwa alikimbia mara baada ya kufyatua risasi hizo, lakini baadaye alikamatwa katika eneo la karibu la Sherman Oaks bila kutoa upinzani wowote.
Polisi pia walifanikiwa kukamata silaha inayodaiwa kutumika katika tukio hilo, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo halisi cha shambulio hilo, kwani mpaka sasa sababu ya mshukiwa kufanya tukio hilo bado haijajulikana.
Baadhi ya majirani wa eneo hilo wamesema milio ya risasi ilileta hofu kubwa katika kitongoji hicho kinachojulikana kwa utulivu na usalama.
Mmoja wa majirani, Keith England, alisema tukio hilo lilikuwa la kutisha sana kutokana na milio ya risasi iliyosikika ghafla.
“Ilikuwa ya kutisha. Siwezi kufikiria kuwa ndani ya nyumba halafu unasikia risasi zikigonga kuta,” alisema jirani huyo.
Aliongeza kuwa risasi zilifyatuliwa kwa mfululizo na kusababisha taharuki kwa wakazi wa eneo hilo.
“Bam, bam, bam zilikuwa kama risasi kumi hivi,” alieleza.
Tukio hilo limewashangaza wengi katika eneo la Beverly Hills, huku polisi wakiendelea na uchunguzi ili kubaini sababu na mazingira yaliyopelekea shambulio hilo.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni