Breaking


Ijumaa, 6 Machi 2026

POLISI NIGERIA WATHIBITISHA SHAMBULIO BORNO

Polisi wa Nigeria wameithibitishia BBC kwamba watu kadhaa kutoka jamii ya Ngoshe katika jimbo la Borno, Nigeria wameuawa na wengine kutekwa nyara na wanaume wenye silaha.

Msemaji wa polisi katika Jimbo la Borno, Nahum Daso Kenneth, ameimbia BBC siku ya Ijumaa kwamba shambulio hilo lilitokea Jumatano usiku lakini akasema bado hawezi kuthibitisha idadi ya watu walioathirika.

Amesema, "operesheni ya utafutaji na uokoaji inaendelea.”

Vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kwamba wanamgambo wamewateka nyara zaidi ya wanawake na watoto 100 wakati wa shambulio hilo. 

Ripoti zinasema washambuliaji hao pia walilenga kambi ya kijeshi iliyo karibu na kambi ya watu waliokimbia makazi yao katika eneo hilo, na kuwaua wanajeshi kadhaa na raia, wakiwemo mkuu wa kijiji hicho na baadhi ya wazee.

Umaru Yakubu Kirawa, mwandishi wa habari wa eneo hilo huko Borno, ameiambia BBC wakazi wamethibitisha watu wengi wameuawa na mamia wametekwa nyara.

Ngoshe ni jamii yenye Waislamu wengi, na inaripotiwa kwamba shambulio hilo lilitokea usiku huku watu wengi wakifungua mfungo wao wa Ramadhani.

Kwa miaka mingi, Jimbo la Borno limekuwa kitovu cha uasi wa Kiislamu nchini Nigeria, huku kukiwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa Boko Haram na wapiganaji wa Kiislamu wa kundi la Dola la Kiislamu Afrika Magharibi (Iswap).

Boko Haram ilipata umaarufu duniani mwaka 2014 baada ya kuwateka nyara zaidi ya wasichana 200 wa shule kutoka Chibok katika jimbo hilo.

Hakuna maoni: