Serikali imechukua hatua za dharura kwa kulielekeza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuagiza mafuta mengi kwa pamoja, ili kuhakikisha usalama na upatikanaji wa mafuta ya kutosha nchini kwa bei himilivu kuanzia mwezi Mei hadi Julai 2026.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio, ambaye amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa mafuta katika soko la kimataifa, zilizochangiwa na vita vinavyoendelea katika ukanda wa Mashariki ya Kati.
Ameeleza kuwa kutokana na hali hiyo, TPDC itanunua mafuta kwa pamoja, hatua itakayosaidia kupata bei nafuu zaidi ikilinganishwa na utaratibu wa awali uliokuwa ukitumika kupitia Wakala wa Ununuzi wa Pamoja wa Mafuta (PBPA), ambapo waagizaji wanakuwa wengi na wanaagiza kwa kiwango kidogo kidogo.
Uamuzi huo unakuja wakati bei za mafuta duniani zikiongezeka kwa kasi zaidi ya mara mbili katika miezi ya hivi karibuni kutoka kati ya dola 50 hadi 60 kwa pipa mwezi Februari hadi takribani dola 114 kwa hivi sasa hali inayoongeza wasiwasi wa kupanda kwa bei ndani ya nchi.
Aidha, Dkt. Mataragio amefafanua kuwa Waziri mwenye dhamana ana Mamlaka ya kutumia Sheria ya Mafuta kuweka utaratibu maalum wa upatikanaji wa mafuta nchini, ili kuhakikisha uwepo wa mafuta ya kutosha na kwa bei nafuu. Kutokana na hali ya sasa, TPDC imeelekezwa kuagiza mafuta yatakayokidhi mahitaji ya kipindi hiki cha changamoto.
Akizungumzia changamoto zilizopo, amesema kuwa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya soko ni vigumu kupata mafuta kwa bei nzuri endapo yataagizwa kwa kiwango kidogo kidogo, kwani gharama huwa kubwa.
“Tulichobaini katika kipindi hiki ni kwamba upatikanaji wa mafuta huwa mgumu pale unapoagiza kwa kiwango kidogo, yaani meli moja moja, hali inayosababisha bei kuwa juu. Ili kupata bei nzuri ni muhimu kuagiza mafuta kwa wingi pamoja na kuwa na mikataba ya muda mrefu,” amesema Mataragio.
Vilevile, ameeleza kuwa TPDC tayari imekwishafanya uchambuzi wa mwenendo wa bei ya mafuta duniani na kubaini kuwa ununuzi wa mafuta mengi kwa pamoja kwa wakati mmoja utasaidia kupata bei ya chini zaidi kuliko kutumia utaratibu wa awali kupitia PBPA.
Dkt. Mataragio pia ameielekeza TPDC kufuatilia kwa karibu mchakato mzima wa uagizaji wa mafuta ili kuhakikisha shehena zote zilizokusudiwa zinafika nchini kwa wakati.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni