Breaking


Alhamisi, 12 Machi 2026

TANZANIA NA UGANDA ZASISITIZA UTEKELEZAJI KWA VITENDO KATIKA KUKUZA USHIRIKIANO WA UWILI

Tanzania na Uganda zimethibitisha tena dhamira yao ya kuimarisha ushirikiano wa uwili, kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya pamoja, na kuibua maeneo mapya ya ushrikiano 

Akifungua  kikao cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kinachofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa idara ya afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ali Bujiku amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Uganda katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Ameeleza kuwa mkutano huo ni fursa kwa wataalamu kufanya tathmini ya utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa katika JPC iliyopita, 2022, kujadili changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji, na kupendekeza njia bora za kuimarisha ushirikiano huo.

“Mjadala wetu leo unaakisi upeo mpana na wa kimkakati wa ushirikiano wetu. Tutajadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo diplomasia, ulinzi na usalama, uhamiaji, kilimo, afya, elimu, utamaduni pamoja na biashara.

Balozi Bujiku pia amegusia umuhimu wa kuboresha miundombinu ya mawasiliano na usafirishaji kati ya Tanzania na Uganda, akitaja miradi ya kimkakati ya kikanda ikiwemo bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki pamoja na barabara na miundombinu mingine ya usafiri ambayo inalenga kuongeza ufanisi wa biashara na kuimarisha ujumuishaji wa kikanda.

Kadhalika, Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Kanali Mstaafu Fred Mwesigye amesisitiza umuhimu wa kutatua changamoto zilizopo na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

“Viongozi wetu wametupa jukumu la kushughulikia masuala haya, watakapokutana tena, tunapaswa kuwa tayari kuwaeleza kwamba tumetatua changamoto zote zilizokuwepo na tumeanzisha maeneo mapya ya ushirikiano,” amesema Balozi Mwesigye.

Balozi Mwesigye pia ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuonesha uongozi madhubuti katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), pamoja na kuteuliwa kwa Mtanzania Balozi Patrick Mbundi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo.Alieleza kuwa hatua hizo zinatoa msukumo mpya katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kukuza maendeleo ya pamoja.

Hakuna maoni: