Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa matarajio ya hali mbaya ya hewa kwa siku tano kuanzia Jumatatu, Machi 2, 2026 saa 9:30 mchana, ikieleza kuwa kwa ujumla hakuna tahadhari iliyotolewa kitaifa. Hata hivyo, angalizo la mvua kubwa limetolewa kwa maeneo machache ya mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora, pamoja na Manyara, ambako kuna uwezekano wa wastani wa kutokea kwa mvua hizo na kiwango cha athari kinachokadiriwa kuwa cha wastani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, athari zinazoweza kujitokeza ni pamoja na baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, hasa katika maeneo ya mabondeni au yenye mifereji isiyoruhusu maji kupita kwa urahisi. Wananchi katika maeneo tajwa wametakiwa kuzingatia tahadhari, kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuchukua hatua za mapema ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
TMA imehimiza umma kuendelea kupata taarifa sahihi kupitia njia zake rasmi za mawasiliano na kusisitiza kuwa itaendelea kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa na kutoa maboresho kadri inavyohitajika. Mamlaka hiyo inatoa huduma za hali ya hewa kwa viwango vya kimataifa (ISO 9001:2015), ikiwa ni pamoja na huduma kwa usafiri wa anga, na imewahakikishia Watanzania kuwa itaendelea kutoa taarifa kwa wakati kwa ajili ya usalama na ustawi wa jamii.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni