Breaking


Jumatatu, 9 Machi 2026

UTABIRI WA HALI YA HEWA KWA SAA 24 ZIJAZO


 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetabiri kuwepo kwa hali ya mawingu pamoja na vipindi vya mvua na ngurumo katika maeneo mbalimbali ya nchi katika kipindi cha saa 24 zijazo kuanzia saa 3:00 usiku wa leo Machi 9, 2026. 


Kwa mujibu wa utabiri huo, baadhi ya maeneo ikiwemo mikoa ya Mtwara, Lindi, Morogoro, Dodoma, Singida pamoja na kanda ya ziwa inayojumuisha Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu yanatarajiwa kushuhudia mvua katika maeneo machache kwa vipindi tofauti.


 Hali kama hiyo pia inatarajiwa katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi pamoja na maeneo ya nyanda za juu kusini ikiwemo Mbeya, Songwe, Ruvuma, Rukwa, Iringa na Njombe.


Aidha, kwa upande wa kanda ya kaskazini inayojumuisha Arusha, Kilimanjaro na Manyara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, hali ya mawingu kiasi na mvua za hapa na pale zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo. Kwa ukanda wa Pwani unaojumuisha mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani pamoja na visiwa vya Mafia, hali ya mawingu na vipindi vya mvua nyepesi inaweza kujitokeza katika maeneo machache. 


TMA pia imeeleza kuwa upepo wa pwani unatarajiwa kuvuma kwa kasi ya takribani kilomita 20 kwa saa, ukitokea kaskazini mashariki katika pwani ya kaskazini na kutoka kaskazini katika pwani ya kusini, huku hali ya bahari ikitarajiwa kuwa na mawimbi madogo.


Katika viwango vya joto, jiji la Dar es Salaam linatarajiwa kuwa na joto la juu la nyuzi joto 31°C na la chini 24°C, wakati Arusha ikitarajiwa kuwa na joto la juu la 24°C na la chini 16°C. Miji mingine kama Dodoma, Mwanza na Kigoma inatarajiwa kuwa na joto la juu linalokaribia nyuzi joto 27°C. 


TMA imeeleza kuwa matarajio ya siku ya Jumatano Machi 11, 2026 yanaonesha kuendelea kwa vipindi vya mvua katika maeneo mengi ya nchi, hivyo wananchi wanashauriwa kufuatilia utabiri wa hali ya hewa ili kupanga shughuli zao kwa usahihi.


Hakuna maoni: