Breaking


Jumamosi, 18 Aprili 2026

BIL. 127.7 ZATUMIKA KUFIKISHA NISHATI VIJIJINI MWANZA

Zaidi ya shilingi bilioni 127.7 zimetumika kupeleka huduma ya nishati safi Vijijini Mkoa wa Mwanza hali iliyochochea ukuaji wa uchumi na kuboreka kwa huduma za kijamii vijijini.

Hayo yamesemwa  na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda wakati wa kikao cha kwanza kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wabia wa Maendeleo katika Sekta ya Nishati (EDPG) ambapo Wakala huo uliwasilisha mpango kazi pamoja na bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkoa wa Mwanza pekee imetoa jumla ya shilingi Bilioni 127.7 ili kutekeleza miradi ya kupeleka umeme hadi vitongojini. Mafanikio haya makubwa yamechangiwa pia na wabia wa maendeleo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB),  Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu amesema kuwa wabia hao wa maendeleo wamekuwa na imani kubwa na fedha wanazotoa katika utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini na ndio maana wanaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia REA katika utekelezaji wa miradi hiyo huku akiahidi kuwa Bodi yake itaendelea kuhakikisha kunakuwa na thamani ya fedha katika miradi inayotekelezwa na REA.

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amesema kuwa Wakala umewasilisha mipango na vipaumbele vyake kwa mwaka ujao wa fedha ili wabia hao waweze kuona maeneo wanayoweza kuendelea kushirikiana na Serikali kupitia REA katika kuendelea kuboresha maisha ya Wananchi.

“Pamoja na kazi kubwa inayofanyika katika kujenga miundombinu ya umeme, lakini lengo la msingi ni mwananchi wa kawaida aweze kuunganishiwa umeme na aweze kupata manufaa ya upatikanaji wa umeme.

Tumewasilisha mipango pamoja na vipaumbele katika bajeti yetu ijayo ambapo ni kuharakisha upatikanaji wa umeme kwenye vitongoji. Tumewapitisha pia wenzetu katika mpango wetu maalum wa kuwezesha na kuharakisha uunganishaji umeme majumbani,” amebainisha Mhandisi Saidy.

Mhandisi Saidy pia ameongeza baadhi ya mipango mingine iliyopangwa kutekelezwa na Wakala kwa mwaka ujao wa fedha ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia vijijini, kuwezesha miradi ya nishati jadidifu na kuongeza ufanisi katika matumizi ya umeme na utumiaji wa umeme katika shughuli za maendeleo.

Mwenyekiti wa Wabia wa Maendeleo katika Sekta ya Nishati (EDPG), Robert Hovde ameipongeza Serikali ya Tanzania kupitia REA kwa kufikisha umeme vijijini.

Hakuna maoni: