Aliyewahi kuwa kocha wa timu mbalimbali za soka nchini, zikiwemo Stand United “Chama la Wana” na Pamba (sasa Pamba Jiji), Athuman Bilali maarufu kama Billo, amefariki dunia, huku chanzo cha kifo chake kikiwa bado hakijafahamika.
Marehemu Billo hadi umauti unamkuta alikuwa mmiliki wa kituo cha michezo pamoja na timu ya wanawake ya Bilo Queens inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania.
Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Leonard Malongo, amethibitisha kifo hicho akieleza kuwa ni pigo kubwa kwa wadau wa soka mkoani Mwanza na nchini kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Malongo, taarifa za awali zinaeleza kuwa kocha huyo aliendelea na majukumu yake ya kawaida ya mazoezi na timu ya Bilo Queens katika Uwanja wa Shule ya Msingi Nyasaka jijini Mwanza hadi jioni ya Aprili 15, 2026.
Hata hivyo, baada ya wachezaji kuondoka, aliachwa akiwa amekaa uwanjani, na baadaye alikutwa amefariki katika eneo hilo asubuhi ya siku iliyofuata.
“Jana alikuwa uwanjani akifanya mazoezi na timu yake, na wachezaji walipokuwa wanaondoka walimwacha amekaa. Asubuhi ndipo alikutwa amefariki hapo hapo. Bado hatujajua chanzo cha kifo, kwani mwili wake umehifadhiwa hospitalini kwa uchunguzi zaidi,” amesema Malongo.
Ameongeza kuwa taarifa zaidi kuhusu chanzo cha kifo pamoja na ratiba ya mazishi zitatolewa baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa kitabibu.
Kifo cha Billo kimeacha pengo kubwa katika maendeleo ya soka, hususan katika kuinua vipaji vya wanawake kupitia timu yake ya Bilo Queens. Wadadau wa michezo wanatarajiwa kuendelea kutoa salamu za rambirambi huku wakikumbuka mchango wake mkubwa katika tasnia ya soka nchini.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni