Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema Mamlaka hiyo itaendelea kupambana na watu wote wanaokwepa kodi ili kuwalinda wafanyabiashara wanaozingatia sheria za kodi.
Akizungumza na walipakodi mkoani Mara Aprili 15, 2026 Kamishna Mkuu Mwenda amesema watu wanaokwepa kodi wamekuwa wakiondoa ushindani wa biashara sokoni hivyo TRA itaendelea kupambana nao na kuwachukulia hatua za kisheria.
"Tutawatafuta popote walipo watu wanaokwepa kodi maana wamekuwa wakiwaumiza walipakodi wanaozingatia sheria, huwezi kukwepa kodi milele, ipo siku tutakukamata. Na ninatoa wito kwa yeyote anayewafahamu watu wanaokwepa kodi awasiliane na TRA ili hatua ziweze kuchukuliwa"
Aidha amewaonya wafanyabiashara wanaojihusisha na uingizaji wa bidhaa za magendo kwenye mpaka wa Sirali na mipaka mingine, na kueleza kuwa TRA ipo kazini kupambana na magendo na itawafikia.
Kuhusu mahusiano na Walipakodi Kamishna Mkuu Mwenda amesema wataendelea kuboresha mahusiano, kuwasikiliza, kutatua changamoto zao pamoja na kuwezesha biashara nchini.
Amesema TRA itaendelea kuongeza wigo wa kodi nchini kwa kusajili walipakodi wapya na hii nimkutokana na nguvu kazi iliyopo nchini kutowiana na idadi ya walipakodi ambao ni Milioni 8 huku nguvu kazi ikiwa ni zaidi ya milioni 30.
Kwa upande wake Kamishna wa Kodi za ndani Bw. Michael Muhoja amesema TRA itaendelea kutoa elimu ya kodi kwa wananchi ili kuwawezesha kutambua umuhimu wa kulipa kodi.
Miongoni mwa walipakodi waliohudhurua mkutano huo wameipongeza TRA kwa kuendelea kuwa karibu nao na kuwapatia elimu ya kodi kila inapohitajika.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni