Ushirikiano baina ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na walipakodi umetajwa kuwezesha mamlaka hiyo kuandika historia mpya kwa kukusanya shilingi trilioni 9.31 katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/26, sawa na ufanisi wa asilimia 106.4 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 8.75.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda tarehe Aprili 1, 2026, mwezi Machi pekee TRA ilikusanya shilingi trilioni 3.58, sawa na ufanisi wa asilimia 107.6 ya lengo la trilioni 3.32.
Makusanyo ya robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/26 yanaonesha ukuaji wa asilimia 23.6 ikilinganishwa na shilingi trilioni 7.53 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2024/25.
Aidha, wastani wa makusanyo kwa mwezi katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025/26 umefikia shilingi trilioni 3.10, kiwango cha juu zaidi kulinganisha na wastani wa shilingi trilioni 2.51 kwa kipindi kama hicho mwaka 2024/25.
TRA pia imefanikiwa kufikia na kuvuka malengo ya makusanyo kwa miezi 21 mfululizo tangu Julai 2024, mafanikio ambayo hayajawahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.
Vilevile, makusanyo ya robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/26 yanaonesha ukuaji wa asilimia 114.1 ikilinganishwa na shilingi trilioni 4.35 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho wakati Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani mwaka 2020/21.
Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, TRA ilisajili walipakodi wapya 900,755, sawa na ufanisi wa asilimia 131.36 ya lengo la kusajili walipakodi 685,706 kufikia tarehe 31 Machi 2026.
Aidha, katika robo ya tatu, mahusiano kati ya TRA na viongozi wa vyama vya wafanyabiashara pamoja na wafanyabiashara yaliimarishwa kupitia mikutano ya kusikiliza na kutatua changamoto za kikodi.
TRA imewahakikishia wananchi na umma kwa ujumla kuwa itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wote ili kuhakikisha malengo ya makusanyo kwa mwaka wa fedha 2025/26 yanafikiwa kikamilifu, hatua itakayoiwezesha Serikali kuendelea kutekeleza mipango ya maendeleo kwa manufaa ya Taifa zima.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni