Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, ameishauri Benki ya Dunia kuangalia namna ya kuiwezesha sekta binafsi katika nchi za Afrika ili iweze kuwa imara na kuchangia kukuza uchumi wa nchi hizo.
Mhe. Balozi Omar, ametoa wito huo wakati akichangia mada katika mkutano wa Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika, wanachama wa Benki ya Dunia (Africa Group 1 Constituency), uliofanyika Makao Makuu ya Benki hiyo, Jijini Washington D.C, nchini Marekani.
Alisema kuwa wakati nchi za Afrika zinatakiwa kuongeza ufanisi katika kukusanya mapato yake ya ndani, sekta binafsi za nchi wanachama wa Benki ya Dunia ikiwezeshwa kikamilifu, inaweza kuvutia mitaji ya ndani sawa na mitaji ya nje.
Mhe. Balozi Omar alieleza kuwa nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na madeni yanayofikia ukomo wa kuendelea kukopa zaidi, hivyo njia ya kujikwamua na changamoto hiyo ni kuongeza makusanyo ya mapato yao ya ndani kwa kutoza kodi kubwa ambazo kwa namna moja au nyingine zinaathiri kundi kubwa la wananchi masikini.
Alihimiza kuandaliwa mpango mkuu wa mageuzi na maendeleo ya bara la Afrika kama ilivokuwa kwa Ulaya kupitia Marshall Plan.
Akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa majukumu ya Benki ya Dunia kwa Kundi la kwanza la Kanda ya Afrika, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Dkt. Zarau Wendelin Kibwe, alisema kuwa Benki ya Dunia inatarajia kukusanya na kutumia dola za Marekani bilioni 100 kuziwezesha nchi wanachama kukabiliana na changamoto za kiuchumi pamoja na kukuza sekta binafsi.
Alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza ujumuishaji kwa kupanua fursa za ajira kwa wanawake, vijana, na jamii zisizopewa kipaumbele huku ikiimarisha ulinzi wa kijamii na ustahimilivu kutokana na mabadiliko ya kiuchumi.
Aidha, Dkt. Kibwe alisema kuwa juhudi hizo kwa pamoja hazilengi tu kuunda ajira, bali pia kuhakikisha ajira hizo ni za uzalishaji, endelevu, na zinapatikana kwa wote kupitia Ajenda ya Ajira katika kubuni miradi (Agri-Connect, Nishati, Afya, na Madini) na kuweka kipaumbele kwenye sekta zinazozaa ajira kwa lengo la kuunda fursa zaidi za ajira kwa vijana.
Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika wanachama wa Benki ya Dunia (Africa Group 1 Constituency) limeundwa na nchi 22 kutoka Ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo ni Tanzania, Botswana, Burundi, Eritrea, Eswatini, Ethiopia, Gambia, Kenya, Lesotho, Liberia, Malawi, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Seychelles, Sierra Leone, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Uganda, Zambia, na Zimbabwe.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni