Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, ametoa wito kwa jamii, taasisi za umma na binafsi kushirikiana kuondoa unyanyapaa wa hedhi na kuhakikisha huduma rafiki za hedhi salama zinapatikana kwa wanawake na wasichana ili kuwawezesha kuishi kwa utu, usalama na heshima.
Dkt. Samizi ameyasema hayo leo Mei 30, 2026 katika maadhimisho ya Siku ya Hedhi Salama Duniani yaliyofanyika wilayani Kasulu mkoani Kigoma, ambapo pamoja na kuhamasisha jamii kuhusu hedhi salama, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya hususan kuboresha mazingira rafiki kwa wanawake na watoto wa kike kupitia ujenzi wa miundombinu ya afya, maji, usafi na mazingira salama ya kujifunzia mashuleni.
Amesema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita umewezesha kupanuka kwa huduma za msingi za afya na kuboresha miundombinu ya vyoo bora mashuleni na katika vituo vya kutolea huduma za afya, hatua ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kulinda afya, utu na heshima ya wanawake pamoja na watoto wa kike nchini.
Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyobebwa na kaulimbiu isemayo “Tushirikiane Kuhakikisha Huduma Rafiki za Hedhi Salama kwa Wanawake na Wasichana” (Together for a Period-Friendly World), Dkt. Samizi amesema hedhi ni mabadiliko ya kawaida ya kibayolojia na si ugonjwa wala jambo la kuaibisha, hivyo jamii inapaswa kuondoa mila potofu na unyanyapaa unaowakwamisha wasichana kushiriki kikamilifu shughuli za kijamii na kielimu.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili wasichana nchini, amesema tafiti zinaonesha kuwa asilimia 27 ya wasichana hukosa shule angalau siku tatu kila mwezi kutokana na maumivu au kutosimamiwa vizuri kwa mahitaji ya hedhi, jambo linalowapotezea zaidi ya siku 30 za masomo kwa mwaka na kuathiri maendeleo yao kitaaluma.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu rafiki ya hedhi salama kwa kujenga vyoo bora vyenye huduma ya maji pamoja na vifaa vya kuhifadhia taka za hedhi katika vituo vya huduma za afya 3,544 nchini. Aidha, shule za msingi 1,849 zimejengewa vyoo bora vyenye vyumba maalumu vya kubadilishia wasichana ili kuhakikisha wanapata mazingira salama na yenye staha.
Sambamba na hilo, Dkt. Samizi amezielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa, hospitali na wadau mbalimbali nchini kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuvunja ukimya na mila potofu kuhusu hedhi, kuhimiza uwekezaji wa miundombinu rafiki katika maeneo ya umma ikiwemo mashine za kuuzia pedi (Vending Machines) na viteketezi vya taka za hedhi (Incinerators), pamoja na kuimarisha huduma za maji safi na vyumba maalum vya kubadilishia kwa ajili ya wasichana.
Aidha, amewashukuru wadau mbalimbali wanaoendelea kushirikiana na Serikali katika kusaidia upatikanaji wa bidhaa za hedhi salama kwa wanawake na wasichana nchini, akitolea mfano mchango wa taulo za kike 7,200 zitakazotolewa katika Jimbo la Mhambwe kwa wanafunzi na wasichana wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na kaya zenye uhitaji.
Dkt. Samizi amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha hakuna mtoto wa kike anayekatishwa ndoto zake kutokana na changamoto za hedhi, huku akitoa rai kwa wabunge na viongozi wengine nchini kuunga mkono afua za hedhi salama katika maeneo yao.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni