SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), limeendelea kuimarisha ulinzi wa rasilimali za Taifa kwa kufanya jumla ya doria 42,941 katika Hifadhi za Taifa 21 nchini hatua iliyosaidia kukamatwa kwa majangili 5,294 waliohusika katika matukio 4,929 ya ujangili.
Takwimu hizo zimetolewa Mei 15,2026,Bungeni na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.Ashatu Kijaji wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2026/2027.
Amesema mbali na kukamatwa kwa majangili hao, doria hizo pia zimefanikiwa kukamata mifugo 59,881 iliyoingizwa ndani ya hifadhi kinyume cha sheria pamoja na silaha 78 zilizokuwa zikitumika katika shughuli haramu.
Aidha, TANAPA imefanikiwa kutegua mitego ya nyaya 9,847 iliyokuwa imetegwa ndani ya maeneo ya hifadhi kwa ajili ya kuwinda wanyamapori kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watuhumiwa wote waliokamatwa wamefikishwa mahakamani huku hatua mbalimbali za kisheria zikiendelea kuchukuliwa dhidi yao.
Katika kuendelea kuimarisha usalama wa wanyamapori, Shirika limeendelea kutumia teknolojia ya kisasa ya visukuma mawimbi ambapo faru 17 wamewekewa alama za masikio huku faru wengine watatu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti wakifungwa vifaa maalum vya ufuatiliaji.
Pia, TANAPA imeendelea kufanya doria kwa kutumia ndege pamoja na ndege nyuki hatua ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kudhibiti matukio ya ujangili katika maeneo ya hifadhi nchini.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni