Breaking


Jumanne, 5 Mei 2026

IMF YAIPONGEZA TRA KWA UFANISI KATIKA USIMAMIZI WA KODI TANZANIA

Shirika la Fedha Duniani (IMF) limeipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuonyesha kiwango kikubwa cha ufanisi katika usimamizi wa ukusanyaji wa kodi, hatua iliyochangia kuongezeka kwa uhiari wa ulipaji kodi pamoja na makusanyo ya serikali katika mwaka wa fedha 2025/26.


Pongezi hizo zimetolewa na ujumbe wa IMF ulioongozwa na Bw. Nicolas Blancher, wakati wa kikao cha mazungumzo na viongozi wa TRA kilichofanyika Mei 4, 2026 katika ofisi za mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam. Katika kikao hicho, TRA iliwakilishwa na Naibu Kamishna Mkuu, Bw. Mcha Hassan Mcha.


Katika majadiliano hayo, IMF ilieleza kuridhishwa na namna TRA inavyotekeleza majukumu yake kwa weledi, hali iliyochangia kuimarika kwa utulivu wa mfumo wa kodi na kupungua kwa malalamiko kutoka kwa walipakodi. IMF ilibainisha kuwa hatua hizo zimeongeza imani kwa walipakodi na kuimarisha nidhamu ya ulipaji kodi nchini.


Aidha, IMF imeahidi kuendeleza ushirikiano wake na TRA kwa kusaidia kujenga uwezo wa watumishi wake katika maeneo mbalimbali, ikiwemo usimamizi wa kodi kwenye sekta ya uzalishaji na viwanda, pamoja na mbinu bora za kurasimisha sekta isiyo rasmi ili kuongeza wigo wa walipakodi.


Katika hatua nyingine, IMF imeeleza kuwa itaiwezesha TRA kupata mafunzo ya kitaalamu katika uendeshaji wa maabara za forodha na utekelezaji wa mikakati ya kuongeza uhiari wa ulipaji kodi, jambo litakalosaidia kuboresha zaidi mifumo ya ukusanyaji mapato.


Kwa upande wake, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Mcha Hassan Mcha, ameishukuru IMF kwa ushirikiano huo, akieleza kuwa utaongeza ufanisi wa watumishi wa TRA na kuboresha utoaji wa huduma kwa walipakodi. Ameongeza kuwa uhusiano wa muda mrefu kati ya TRA na IMF umeendelea kuleta matokeo chanya katika utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo.


Ushirikiano huu unatarajiwa kuimarisha zaidi sekta ya ukusanyaji mapato nchini na kuchangia maendeleo ya uchumi kwa ujumla kupitia mifumo madhubuti ya kodi.


Hakuna maoni: