Breaking


Jumanne, 5 Mei 2026

RC MTANDA AYAANIKA MAFANIKIO SEKTA YA AFYA MWANZA: ZAIDI YA BILIONI 49 ZAWEKEZWA


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, ametoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta ya afya, akieleza kuwa umeleta mageuzi makubwa ya huduma za matibabu mkoani humo.

Akizungumza Mei 4, 2026 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Jua Namba Zako”, Mtanda amesema kuwa hadi kufikia mwaka 2025, Mkoa wa Mwanza umepokea jumla ya shilingi bilioni 49.46 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya afya. Kiasi hicho ni zaidi ya mara mbili ya shilingi bilioni 21.96 zilizotolewa mwaka 2020, jambo linaloonyesha ongezeko kubwa la uwekezaji wa serikali katika sekta hiyo muhimu.

Kupungua kwa Vifo vya Mama na Mtoto

Mtanda ameeleza kuwa uwekezaji huo umeanza kuzaa matunda, ambapo kumekuwa na upungufu wa vifo vya akina mama wajawazito pamoja na watoto wachanga. Takwimu zinaonyesha kuwa vifo vya akina mama vimepungua kutoka 171 mwaka 2020 hadi 165 kufikia Desemba 2025.

Aidha, vifo vya watoto wachanga vimeshuka kutoka 859 hadi 720 katika kipindi hicho, hali inayodhihirisha kuimarika kwa huduma za afya ya uzazi na mtoto.

Ongezeko la Watumishi wa Afya

Katika hatua nyingine, idadi ya watumishi wa afya imeongezeka kwa kiwango kikubwa kutoka watumishi 2,500 mwaka 2020 hadi kufikia 6,564 kwa sasa. Ongezeko hilo limeongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kupunguza changamoto ya uhaba wa wataalamu wa afya.

Mapato ya Vituo vya Afya Yaongezeka

Mkuu huyo wa mkoa pia amebainisha mafanikio katika ukusanyaji wa mapato kupitia mfumo wa kisasa wa GoT-HoMIS, ambapo vituo vya kutolea huduma za afya vinavyotumia mfumo huo vimeongezeka kutoka 26 hadi kufikia 339.

Matumizi ya mfumo huo yamewezesha mkoa kufikia asilimia 94.7 ya utekelezaji, hatua inayochangia uwazi na ufanisi katika usimamizi wa mapato ya sekta ya afya.

Mafanikio katika Bima ya Afya

Kwa upande wa bima ya afya, Mwanza imeendelea kufanya vizuri kitaifa kwa kuwa miongoni mwa mikoa mitatu bora. Mkoa huo tayari umefanikiwa kuandikisha kaya 13 kati ya 19, huku ukiendelea na kampeni kabambe ya kuhamasisha wananchi kujiunga na huduma za bima ya afya.

Huduma za Matibabu ya Homa ya Ini

Akizungumzia huduma za magonjwa sugu, Mtanda amesema kuwa katika kipindi cha Januari hadi Aprili 2026, jumla ya wagonjwa 523 wa Hepatitis B na wagonjwa 78 wa Hepatitis C wanaendelea kupatiwa matibabu katika vituo vya afya vya mkoa huo.


Hakuna maoni: