Breaking


Jumatatu, 4 Mei 2026

KAMISHENI YARIDHISHWA NA KASI YA UKUSANYAJI WA MADUHULI, TUME YA MADINI

 

Kamisheni ya Tume ya Madini imeridhishwa na kasi ya ukusanyaji wa maduhuli katika sekta ya madini, hatua inayotoa matarajio ya Serikali kuvuka lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Dkt. Janet R. Lekashingo, alipokuwa akiongoza kikao cha Kamisheni jijini Dodoma kilicholenga kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa kipindi cha miezi mitatu.

Mafanikio yaongezeka katika sekta ya madini

Katika kikao hicho, Dkt. Lekashingo aliwapongeza watendaji wa Tume kwa mafanikio yaliyopatikana, ikiwemo kuongezeka kwa ukusanyaji wa maduhuli, usimamizi bora wa masoko ya madini pamoja na vituo vya ununuzi, na kuimarika kwa usalama migodini.

“Kwa kasi iliyopo, tuna imani ya kuvuka lengo la Serikali la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka huu wa fedha,” amesema Dkt. Lekashingo.

Aidha, ameongeza kuwa hatua hizo zinaonesha dhamira ya dhati ya kukuza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa.

Usimamizi wa leseni na biashara ya madini waimarika

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, amesema katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita Tume imeendelea kusimamia utoaji na ufuatiliaji wa leseni za madini, uzalishaji, mauzo pamoja na ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.

Ameeleza kuwa kaguzi zimefanyika katika migodi mikubwa, ya kati na midogo, pamoja na mitambo ya uchakataji, mabwawa ya tope sumu na maeneo ya miambataka, kwa lengo la kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa kuzingatia usalama, afya na mazingira.

Masoko ya madini yaongeza uwazi

Tume pia imeendelea kuimarisha usimamizi wa biashara ya madini kupitia masoko 44 ya madini na vituo 120 vya ununuzi vilivyoanzishwa nchini, hatua iliyosaidia kuongeza uwazi na mapato ya Serikali.

Msisitizo kwenye madini mkakati na teknolojia

Katika hatua ya kimkakati, Kamisheni imesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika mafunzo ya kisasa kwa watumishi wa Tume ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la kimataifa, hasa katika usimamizi wa madini mkakati kama vile lithium, nickel na cobalt.

Imeelezwa kuwa Tanzania inapaswa kujiandaa kunufaika na rasilimali hizi muhimu katika uchumi wa dunia unaoelekea kwenye nishati safi na teknolojia za kisasa.

Kuimarisha uwezo wa watumishi

Kamisheni imependekeza mafunzo endelevu yatakayolenga kuwajengea watumishi uwezo katika:

  • uchambuzi wa data za kijiolojia
  • matumizi ya teknolojia za kidijitali
  • ufuatiliaji wa minyororo ya thamani ya madini
  • mifumo ya kisasa ya kudhibiti biashara na utoroshaji

Hatua hii inalenga kuwabadilisha watumishi kuwa wasimamizi wabunifu (proactive regulators) badala ya wasimamizi wa kawaida (reactive regulators).

Mikakati ya kukuza sekta

Katika kikao hicho, Kamisheni pia ilijadili changamoto zinazoikabili sekta ya madini na kuweka mikakati kupitia kamati mbalimbali ikiwemo za Ufundi, Rasilimali Watu, Fedha na Ushirikishwaji wa Watanzania.

Kwa upande mwingine, Dkt. Lekashingo amewataka watendaji kuendelea kuimarisha tafiti za madini mkakati na kudhibiti utoroshaji wa madini ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi.


Hakuna maoni: