Serikali imeanza kuona matokeo chanya ya mageuzi ya kidijitali katika sekta ya habari, baada ya jumla ya waandishi wa habari 3,357 kuthibitishwa na kupatiwa ithibati ndani ya kipindi cha chini ya mwaka mmoja kupitia mfumo wa kisasa wa TAI HABARI.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni mafanikio makubwa katika kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari nchini, hasa katika kuongeza uwajibikaji, weledi na usimamizi wa sekta hiyo. Kwa mara ya kwanza, sekta ya habari imeanza kutumia mfumo rasmi wa kidijitali unaorahisisha uchakataji wa maombi na uhakiki wa waandishi wanaokidhi vigezo vilivyowekwa kisheria.Akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa wizara hiyo, Paul Christian Makonda, alisema kuwa kuanzia Julai 2025 hadi Aprili 2026, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imepokea jumla ya maombi 4,139 kupitia mfumo wa TAI HABARI.Alifafanua kuwa kati ya maombi hayo, waandishi 3,357 walikidhi vigezo vilivyobainishwa katika Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, na hivyo kupatiwa ithibati rasmi.Katika hatua nyingine, Waziri Makonda alisema JAB pia imeshughulikia malalamiko 14 yanayohusu uvunjifu wa maadili ya taaluma ya habari, hatua inayoashiria kuimarika kwa mifumo ya uwajibikaji ndani ya sekta hiyo.Aidha, serikali kupitia JAB imeandaa mwongozo maalumu wa kisheria utakaowawezesha waandishi wa habari wakongwe ambao walikumbwa na changamoto katika mfumo wa ithibati kurejea rasmi. Mwongozo huo unazingatia masharti ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, ambayo inalenga kukuza na kulinda taaluma ya uandishi wa habari nchini.Kwa mujibu wa Waziri Makonda, mwongozo huo utawezesha kutambua na kuthibitisha umahiri wa waandishi hao kupitia tathmini ya uzoefu, weledi na maadili ya taaluma, na hatimaye kuwapatia ithibati kwa mujibu wa sheria.Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa hata waandishi wenye uzoefu mkubwa wanapata fursa ya kuwa sehemu ya mfumo rasmi unaotambuliwa kisheria, huku ikiimarisha ubora wa habari zinazotolewa kwa umma.Mageuzi haya ya kidijitali kupitia mfumo wa TAI HABARI yanaashiria mwelekeo mpya wa sekta ya habari nchini Tanzania, ambapo uwazi, weledi na usimamizi bora vinapewa kipaumbele. Mfumo huo unatarajiwa kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa waandishi wa habari pamoja na kulinda maslahi ya umma kwa ujumla.








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni