Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Lameck Karanga, alisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha vijana katika uhifadhi wa urithi wa taifa. Alieleza kuwa kuwajengea uelewa mapema kutasaidia kulinda na kuendeleza utamaduni wa Tanzania, huku akitoa wito kwa jamii na wadau kushiriki kikamilifu katika kulinda maeneo ya urithi na kubuni maeneo mapya yatakayoongeza thamani ya kipekee kimataifa (Outstanding Universal Value).
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii Ngorongoro, Joas Makwati, alisema juhudi zinaendelea kuimarishwa ili kuhifadhi na kuitangaza Ngorongoro kimataifa. Alibainisha kuwa eneo hilo lina umuhimu mkubwa wa kisayansi, hasa kutokana na ushahidi wa historia ya mwanadamu uliopatikana katika Bonde la Olduvai, ambako masalia ya binadamu wa kale na zana za mawe vimegunduliwa.
Naye Naibu Katibu wa Tume ya Taifa ya UNESCO Tanzania, Dkt. Khamis Said, alieleza kuwa tangu Tanzania ijiunge na UNESCO, nchi imepata mafanikio makubwa ikiwemo kuridhia mikataba 10 ya shirika hilo, kuwa na Hifadhi Hai sita za Mwanadamu na Mazingira (Biosphere Reserves), pamoja na maeneo saba ya Urithi wa Dunia.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Kusherekea Urithi wa Afrika na Kukuza Viongozi wa Baadaye” (Celebrating Africa’s Heritage, Mentoring the Leaders of Tomorrow), ikisisitiza umuhimu wa kuwaandaa vijana kuwa walinzi na mabalozi wa urithi wa bara la Afrika.
Maadhimisho haya yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuelimisha jamii, hususan kizazi kipya, kuhusu thamani ya urithi wa dunia. Kwa kuwekeza katika elimu na uhamasishaji, Tanzania inaweka msingi imara wa kulinda rasilimali zake za kihistoria na kiutamaduni kwa manufaa ya vizazi vijavyo pamoja na kukuza utalii endelevu.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni