Ziara za marais wawili, Paul Kagame wa Rwanda, na Kenya, William Ruto, nchini Tanzania, zimeibua mjadala mzito wa kiuchumi na kisiasa katika ukanda wa Afrika Mashariki, wengi wanajiuliza: Je, ujio huu unaashiria nini?, ni Diplomasia ya kawaida au ni uthibitisho wa kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
DIPLOMASIA YA UCHUMI INAONGEZEKA
Kwa mtazamo wa haraka, ziara hizi si za kawaida, ni sehemu ya kile kinachoitwa economic diplomacy, ambapo viongozi wanatumia mahusiano ya kisiasa kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo ya pamoja.
Taarifa zinaonesha kuwa ziara hizi zinalenga kuimarisha ushirikiano katika sekta za biashara, miundombinu, nishati, afya na elimu, hii inaashiria kuwa Tanzania imeendelea kuwa kitovu muhimu cha uchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki-EAC.
TANZANIA KAMA KITOVU CHA BIASHARA EAC
Uchambuzi unaonesha kuwa Tanzania inazidi kujijenga kama lango la biashara kwa nchi zisizo na bandari kama Rwanda na hata Uganda. Bandari ya Dar es Salaam na miradi ya reli vinaifanya Tanzania kuwa mhimili wa usafirishaji wa bidhaa.
Hii ni kwa mujibu wa mchambuzi Timoth Lyanga, ambaye ni Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, akichambua kwa kina kuhusu ujio wa viongozi hao wawili nchini Tanzania.
Takwimu zinaonesha biashara kati ya Kenya na Tanzania inachangia karibu asilimia 40 ya biashara yote ndani ya EAC (2020–2024).
Biashara kati ya Tanzania na Rwanda inaendelea kukua kwa kasi, ikichochewa na uwekezaji wa pande zote mbili.
FURSA ZA AJIRA: WANANCHI WANAFAIDIKA VIPI?
Uwekezaji wa kampuni za Kenya nchini Rwanda pekee uliwahi kuajiri maelfu ya watu, hii ina maana kuwa ushirikiano wa kikanda unachochea ajira kwa pande zote.
Aidha, ziara za Rais Kagame na Rais Ruto nchini Tanzania si za kawaida, ni ujumbe mzito wa kiuchumi na zinathibitisha mambo matatu makubwa, ambapo Tanzania imeimarika kidiplomasia chini ya Rais Dkt.Samia, Mazingira ya uwekezaji yanazidi kuvutia ndani ya EAC na Ushirikiano wa kikanda sasa unalenga matokeo ya moja kwa moja-biashara, uwekezaji na ajira.
Kwa lugha rahisi, Tanzania kwa sasa si tu mshiriki wa EAC, bali ni kitovu kinachovuta uchumi wa ukanda mzima.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni