Breaking


Jumatano, 6 Mei 2026

REA YAWEZESHA VIKOSI VYA JKT KUKUZA MATUMIZI YA NISHATI SAFI

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini-REB, Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu ametoa wito kwa vikosi vya Jeshi la Kujenga Taifa-JKT vilivyopata miradi ya nishati safi ya kupikia kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa jamii zinazowazunguka.

Mwenyekiti Kingu, ametoa wito huo wakati wa ziara ya bodi hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia inaayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini-REA katika Kambi ya JKT ya Maramba, mkoani Tanga.

Aidha, amesisitiza vijana wanaliopo kwenye kambi hizo za JKT kupatiwa mafunzo ya namna ya kutengeneza mkaa mbadala ili waweze kutumia ujuzi huo kujiajiri na kuwa mawakala wa kutengeneza mkaa mbadala pindi watakapomaliza mafunzo yao.

Kwa upande wake, akimwakilisha Mkuu wa JKT, Kanali Projest Rutaihwa, aliishukuru menejimenti na Bodi ya REA kwa utekelezaji wa miradi nishati safi ya kupikia huku akiahidi kusimamia mradi huo unakuwa endelevu ili kuendelea kulinda mazingira pamoja na afya za wanaoandaa chakula.

Naye, Luteni Kanali Thobias Ngailo, Meneja wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka JKT, ameeleza kuwa vikosi 22 vimenufaika na fedha zilizotolewa na Serikali kupitia REA, ambapo mashine 30 kati ya 60 za kutengeneza mkaa mbadala zimeshasambazwa katika vikosi na zinaendelea kufanya kazi, hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji na matumizi ya nishati safi kwa kiwango kikubwa.

Hakuna maoni: