Mashindano ya Kombe la Dunia mwaka huu yataandaliwa kwa ushirikiano kati ya United States, Canada na Mexico, huku fainali hiyo ikitarajiwa kuvutia mamilioni ya watazamaji duniani kote. Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, burudani hiyo ya mapumziko itadumu kwa takribani dakika 11 na kuwa ya kwanza kufanyika katika historia ya fainali za Kombe la Dunia.
Kwa miaka mingi, maonyesho ya muziki kabla ya mechi yamekuwa sehemu ya mashindano makubwa kama UEFA Champions League Final, lakini FIFA sasa inaongeza burudani ya kiwango kikubwa zaidi wakati wa mapumziko ya mchezo wenyewe. Hatua hiyo inalenga kuongeza thamani ya burudani na kuwapa mashabiki uzoefu wa kipekee ndani na nje ya uwanja.
Shakira anatarajiwa kuwasilisha wimbo rasmi wa Kombe la Dunia uitwao Dai Dai, ambao pia utamshirikisha msanii wa Nigeria Burna Boy. Msanii huyo tayari ana historia kubwa kwenye mashindano hayo baada ya kutamba na wimbo wa Waka Waka (This Time for Africa) wakati wa Kombe la Dunia 2010 lililofanyika nchini South Africa.
Kwa upande wake, Madonna ambaye anajulikana kama “Malkia wa Pop”, anatarajiwa kutumia jukwaa hilo kutangaza albamu yake mpya Confessions II inayotarajiwa kutoka Julai 3. Nao BTS wanaendelea kuweka rekodi kubwa katika muziki wa Korea Kusini, huku kundi hilo likitajwa kuwa miongoni mwa makundi yenye mafanikio makubwa duniani kwa mauzo ya albamu na umaarufu wa kimataifa.
Rais wa FIFA, Gianni Infantino, amesema onyesho hilo litakuwa sehemu ya historia mpya ya Kombe la Dunia na moja ya matukio makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika michezo duniani. Maandalizi ya burudani hiyo yanaongozwa na Chris Martin wa kundi la Coldplay, huku tukio hilo pia likitarajiwa kusaidia kuchangisha fedha kwa ajili ya mfuko wa elimu wa FIFA unaolenga kusaidia watoto duniani kote.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni