Mahakama nchini Nigeria imemhukumu aliyekuwa Waziri wa Nishati, Saleh Mamman, kifungo cha miaka 75 jela baada ya kupatikana na hatia ya kutakatisha fedha kiasi cha naira bilioni 33.8, sawa na dola milioni 24.7 za Marekani.
Hukumu hiyo ilitolewa Jumatano katika mji mkuu wa Abuja, huku mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 68 akitajwa kutokuwepo mahakamani wakati wa uamuzi huo.
Awali mwezi huu, mahakama ilimpata Mamman na hatia katika makosa 12 yanayohusiana na udanganyifu pamoja na utakatishaji fedha, kufuatia kesi iliyofunguliwa na Economic and Financial Crimes Commission (EFCC).
Mahakama pia iliamuru arejeshe naira bilioni 22 zinazodaiwa kuhusishwa na miradi ya umeme ya Mambilla na Zungeru aliyokuwa akiisimamia alipokuwa madarakani.
Ripoti zinaeleza kuwa vifungo hivyo vitatumikiwa kwa mfululizo, huku Mamman akitajwa kutofahamika alipo kwa sasa na bado hajatoa tamko lolote kuhusu hukumu hiyo.
Kabla ya hukumu kutolewa, alikuwa amechukua fomu za kuwania uteuzi wa uchaguzi wa ugavana katika jimbo la Taraba kupitia chama tawala cha All Progressives Congress kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027.
Saleh Mamman aliwahi kuhudumu chini ya utawala wa rais wa zamani wa Nigeria, Muhammadu Buhari, ambaye serikali yake iliingia madarakani kwa ahadi ya kupambana na ufisadi.
Hukumu hiyo imeibua mjadala mkubwa nchini humo, huku wengi wakisema kuwa kuwajibishwa kwa viongozi waandamizi kwa makosa ya ufisadi bado ni jambo nadra.
Kesi hiyo ni sehemu ya kampeni kubwa ya EFCC dhidi ya maafisa wa zamani wa serikali wanaotuhumiwa kwa ufisadi.
Uchunguzi mwingine pia umehusisha aliyekuwa Waziri wa Sheria, Abubakar Malami, pamoja na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kibinadamu, Sadiya Umar Farouq, ambaye ameripotiwa kutafutwa na shirika hilo.
Hukumu hiyo pia imefufua hasira za wananchi kuhusu changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa umeme nchini Nigeria.
Licha ya taifa hilo kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa nishati barani Afrika, bado linakabiliwa na uhaba mkubwa wa umeme na kukatika mara kwa mara kwa huduma hiyo, hali inayowaathiri wananchi na biashara nyingi kote nchini.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni