
Waziri wa Maliasili na Utalii,Dkt. Ashatu Kijaji, amesema Serikali itaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya migongano kati ya binadamu na wanyamapori kwa kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kusimamia Utatuzi wa Migongano hiyo kwa kipindi cha mwaka 2025/2026 hadi 2035/2036.
Akiwasilisha mpango wa Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni, Dkt. Kijaji amesema miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na ujenzi wa vituo 30 vya askari katika maeneo yenye changamoto kubwa ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Amesema Wizara kupitia taasisi zake pia itajenga vizimba 72 katika maeneo yanayokumbwa na changamoto ya mamba na viboko pamoja na kuchimba mabwawa 30 ndani ya maeneo ya hifadhi ili kusaidia kudhibiti mienendo ya wanyamapori hao.
Katika kuimarisha matumizi ya teknolojia, Waziri huyo amesema Serikali itanunua ndege nyuki 100 pamoja na visukuma mawimbi 100 kwa ajili ya kufuatilia mienendo ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Aidha, amesema Wizara itanunua mabomu baridi 50,000 na virushio 252 vitakavyotumika kudhibiti wanyamapori hao bila kuwasababishia madhara makubwa.
Kwa upande wa doria na ulinzi, Dkt. Kijaji amesema Serikali itanunua magari 11 ya doria pamoja na kukamilisha ununuzi wa helikopta mbili kwa lengo la kuimarisha ulinzi na udhibiti wa wanyamapori katika maeneo mbalimbali nchini.
Hatua hizo zinatarajiwa kusaidia kupunguza madhara yanayosababishwa na wanyamapori kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi pamoja na kuimarisha usalama wa watu na mali zao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni