Breaking


Alhamisi, 14 Mei 2026

SHINYANGA YAPAA KWA UCHIMBAJI WA DHAHABU NA ALMASI, YAVUTIA UWEKEZAJI WA VIWANDA

Mkoa wa Shinyanga umeendelea kujiimarisha kama moja ya maeneo muhimu ya uzalishaji wa madini nchini, huku shughuli za uchimbaji wa dhahabu na almasi zikichangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi wa mkoa huo. Ukuaji huo pia umefungua fursa mpya za uwekezaji katika viwanda vya kuongeza thamani ya madini na sekta nyingine zinazotegemea rasilimali za asili.

Akizungumza mkoani Shinyanga, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa huo, Mhandisi Noel Odera, amesema mkoa huo umebarikiwa kuwa na rasilimali mbalimbali za madini ikiwemo dhahabu, almasi, madini ya ujenzi pamoja na madini ya viwandani kama chokaa. Amesema rasilimali hizo zimeendelea kuchochea shughuli za kiuchumi, kuongeza ajira kwa wananchi pamoja na kukuza mapato ya Serikali.

Uzalishaji wa dhahabu na almasi waongezeka

Mhandisi Odera amesema shughuli za uchimbaji zinaendelea kufanyika kwa kasi katika maeneo mbalimbali ya Shinyanga zikihusisha wachimbaji wadogo, wa kati pamoja na migodi mikubwa. Baadhi ya migodi hiyo ni pamoja na El-Illari na Williamson Diamond iliyopo Wilaya ya Kishapu, eneo linalotajwa kuwa miongoni mwa maeneo yanayozalisha kiwango kikubwa cha almasi nchini.

Aidha, amesema tafiti mpya zimeongeza matumaini ya kuongezeka kwa uzalishaji wa almasi baada ya wachimbaji wadogo kugundua madini hayo katika eneo la Ng’wapangabule kwenye mwamba unaofanana na kimbaritiki. Hatua hiyo inaelezwa kufungua fursa mpya za uwekezaji pamoja na tafiti zaidi za kijiolojia.

Kwa upande wa dhahabu, amesema uzalishaji unaendelea kuimarika katika maeneo ya Mwakitoryo, Nyandolwa, Mwanubi, Ishinabulandi na Mwazezema, ambapo wachimbaji wadogo na wa kati wamekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza ajira, kipato cha wananchi pamoja na mapato ya Serikali.

Fursa mpya za viwanda vya kuongeza thamani

Mbali na uchimbaji wa madini, Mkoa wa Shinyanga umetajwa kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji katika viwanda vya kisasa vya uchenjuaji wa dhahabu vinavyotumia teknolojia za Carbon in Pulp (CIP) na Carbon in Leach (CIL). Teknolojia hizo zinatarajiwa kusaidia kuongeza thamani ya madini kabla ya kuuzwa na kuboresha huduma za uchenjuaji kwa wachimbaji.

Mhandisi Odera pia amesema mkoa huo una nafasi kubwa ya uwekezaji katika viwanda vya utengenezaji wa vito vya thamani na bidhaa zitokanazo na almasi, hatua itakayosaidia kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi na kukuza uchumi wa viwanda.

Ameongeza kuwa uwepo wa malighafi za kutosha kama chokaa umeifanya Shinyanga kuwa eneo lenye uwezo mkubwa wa uwekezaji katika viwanda vya saruji, jambo litakalosaidia kukuza sekta ya ujenzi, kuongeza ajira na kuimarisha maendeleo ya kijamii.

Serikali yaendelea kuboresha mazingira ya biashara

Kwa mujibu wa Mhandisi Odera, masoko ya madini mkoani humo yanaendelea kuimarika ambapo kwa sasa kuna wanunuzi wakubwa 19 wa dhahabu na almasi wanaofanya biashara Shinyanga. Hali hiyo imeendelea kurahisisha biashara ya madini kwa wachimbaji na kuongeza uwazi katika sekta hiyo.

Amehitimisha kwa kuwahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa zilizopo Shinyanga kwa kuwekeza katika uchimbaji, utafiti wa madini pamoja na viwanda vya kuongeza thamani ya madini. Amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayosaidia sekta ya madini kuchangia zaidi maendeleo endelevu ya taifa na ustawi wa wananchi.


Hakuna maoni: