Breaking


Jumatatu, 4 Mei 2026

TANZANIA NA UTURUKI ZASAINI MIKATABA KUONDOSHA UTOZAJI WA KODI MARA MBILI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Uturuki zimesaini Mikataba miwili ya Kuondoa Utozaji wa Kodi Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji wa Kodi katika Mapato (DTA), hatua inayotarajiwa kuchochea uwekezaji na biashara kati ya mataifa hayo mawili.

Akizungumza katika hafla ya utiaji Saini wa Mkataba huo iliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), alisema kuwa mkataba huo ni wa Kumi na Tatu (13) kwa Tanzania na mataifa mbalimbali na unalenga kuongeza imani kwa wawekezaji kwa kuondoa hatari ya mapato kutozwa kodi mara mbili katika nchi mbili tofauti.

Mhe. Balozi Omar alisisitiza kuwa, mikataba ya aina hiyo inapounganishwa na mikataba ya kulinda uwekezaji (BITs), huwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi kupitia kuimarisha mtiririko wa uwekezaji na biashara.

“Tafiti zinaonesha nchi zenye mikataba madhubuti ya kodi mara mbili huvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (Foreign Direct Investment-FDI) kwa kiwango kikubwa zaidi, hali inayoiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuvutia mitaji kutoka Uturuki na mataifa mengine” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aidha Mhe. Balozi Omar alibainisha kuwa, licha ya Tanzania na Uturuki kuwa na mkataba wa kulinda uwekezaji tangu mwaka 2011, kukosekana kwa Mkataba wa Kuondoa Utozaji Kodi Mara Mbili, kulikuwa pengo ambalo sasa limezibwa na hatua hiyo inatoa ujumbe wa wazi kwa wawekezaji wa Uturuki kuwa Tanzania iko tayari kupokea na kuendeleza biashara.

Aliongeza kuwa, uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili umeendelea kukua hasa kufuatia ziara ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Uturuki mwaka 2024, ambapo biashara kati ya nchi hizo ilifikia dola za Marekani milioni 281.68, huku Uturuki ikisafirisha bidhaa nyingi zaidi ikilinganishwa na Tanzania.

“Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara kupitia mageuzi mbalimbali ikiwemo kurahisisha usajili wa biashara, kidijitali mifumo ya kodi na forodha, pamoja na maboresho ya sheria za ardhi, ajira na utatuzi wa migogoro ya kibiashara na juhudi hizi zimeanza kuzaa matunda, huku Tanzania ikitajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuvutia uwekezaji katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara” alisema Mhe. Balozi Omar

Kwa Upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Said Shaib Mussa, alisema Tanzania na Uturuki zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na wenye tija tangu kuanzishwa rasmi kwa mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1963 na kwa miongo kadhaa, ushirikiano huo umeendelea kupanuka na kugusa sekta mbalimbali muhimu ikiwemo biashara, uwekezaji, elimu, afya, usafirishaji, ulinzi pamoja na maendeleo ya kijamii.

Mhe. Balozi Mussa alisema utiaji wa Saini wa Mikataba hiyo ni hatua muhimu ya kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya ushirikiano wa pande mbili yaliyosainiwa mwaka 2025, kufuatia ziara ya kihistoria ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Uturuki mwaka 2024.

“Lengo kuu ni kubadilisha makubaliano ya kisiasa kuwa matokeo halisi kwa kuweka mkakati wa pamoja wa biashara na uwekezaji wenye thamani ya dola bilioni moja, na baada ya utiaji Saini utafuata mkutano wa Tume ya Pamoja ambao unatoa fursa ya kupitia utekelezaji, kubaini maeneo mapya ya kipaumbele na kuimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati kama viwanda, kilimo, utalii, nishati na maendeleo ya rasilimali watu” Alisema Mhe. Balozi Mussa

Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Dkt. Bekir Gezer,amesema kuwa Mikataba hiyo itasaidia kuimarisha zaidi ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

Tukio hilo lilihudhuriwa pia na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya na Kaimu Naibu Katibu Mkuu, Bw. Rished Bade pamoja na Wakuu wa Idara na Wataalam wengine kutoka Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kutoka Uturuki.

Hakuna maoni: