Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imefanikiwa kupata dola milioni 65 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya dharura ya matengenezo ya miundombinu ya barabara nchini kupitia Mfuko wa Dharura wa CERC.
Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff, wakati wa ziara ya wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya wakala huo katika mradi wa ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 22 pamoja na barabara za maingilio zenye urefu wa mita 290 kwenye barabara ya Ndovelwa yenye urefu wa kilomita 20.2 katika Manispaa ya Tabora.
Mhandisi Seff amesema fedha hizo ni mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia, uliotolewa kufuatia tathmini ya uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mvua za El-Nino mwaka 2024. Alisema tathmini hiyo ilibaini kuwepo kwa maeneo mengi ya barabara yaliyoharibiwa, hali iliyohitaji matengenezo ya haraka ili kurejesha huduma za usafiri na mawasiliano kwa wananchi.“Miradi hii inatekelezwa nchi nzima na kwa wastani utekelezaji wake umefikia asilimia 70. Kazi zote zinatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 2026,” amesema Mhandisi Seff.
Aidha, amesema miradi hiyo inatekelezwa na makandarasi wazawa, jambo ambalo linaendelea kutoa fursa za ajira na kukuza sekta ya ujenzi nchini. Pia amewataka Mameneja na wasimamizi wa TARURA kuongeza usimamizi wa karibu ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa ubora na viwango vinavyotakiwa.
Akizungumzia mradi wa daraja la Ndovelwa, Mhandisi Seff amesema ameridhishwa na maendeleo ya kazi pamoja na ubora wa ujenzi unaoendelea. Amesisitiza kuwa miundombinu hiyo inapaswa kuwa imara na kupitika katika misimu yote ya mwaka ili kuwawezesha wananchi kufikia masoko, shule na kusafirisha pembejeo za kilimo kwa urahisi.Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TARURA, Bi. Nunu Mangu, amesema ujenzi wa daraja na barabara hizo utasaidia kuimarisha mawasiliano na usafiri kwa wananchi wa maeneo husika, hasa kipindi cha mvua.
Pia amewataka wananchi kushiriki katika kuitunza miundombinu hiyo kwa kuwa Serikali kupitia TARURA inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika kuboresha sekta ya usafiri na mawasiliano nchini.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni