Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, waogeleaji hao walikuwa wakijaribu kuchunguza mapango yaliyopo chini ya bahari katika kina cha takriban mita 50 wakati ajali hiyo ilipotokea. Jeshi la Maldives limesema mwili mmoja tayari umepatikana ndani ya pango lililopo mita 60 chini ya maji, huku waokoaji wakiendelea na juhudi za kuwatafuta wengine wanne wanaoaminika bado wako eneo hilo.
Maafisa wa uokoaji wameeleza kuwa operesheni hiyo ni ngumu na yenye hatari kubwa kutokana na kina cha maji pamoja na hali mbaya ya hewa iliyokuwa ikishuhudiwa eneo hilo. Serikali ya Maldives pia ilitoa onyo la njano kwa boti za abiria na wavuvi kufuatia mawimbi makubwa na upepo mkali ulioripotiwa karibu kilomita 100 kusini mwa mji mkuu wa Malé.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, Waitaliano hao waliingia majini Alhamisi asubuhi kwa shughuli za utalii wa kupiga mbizi kabla ya kutoweka. Wafanyakazi wa boti waliokuwa wakisafiri nao walitoa taarifa baada ya kundi hilo kushindwa kurejea juu ya maji kwa muda uliotarajiwa.
Tukio hilo linaelezwa kuwa moja ya ajali kubwa zaidi kuwahi kutokea katika sekta ya scuba diving nchini Maldives, taifa ambalo hutegemea kwa kiasi kikubwa utalii wa baharini na visiwa vya matumbawe kuvutia wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni