Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Hamad Yussuf Masauni amesema msimu ujao wa Ligi ya Muungano utaboreshwa zaidi, ikiwemo kuongeza thamani ya zawadi kwa bingwa ili kuipa hadhi na mvuto mkubwa zaidi ligi hiyo.
Mhe. Masauni amesema lengo la maboresho hayo ni kuifanya Ligi ya Muungano kuwa miongoni mwa ligi bora Afrika Mashariki huku ikiendelea kuwa chachu ya kuimarisha mshikamano na umoja wa Watanzania kupitia michezo.
Ameyasema hayo Mei 24, 2026 mjini Unguja wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo na zawadi kwa washiriki wa Ligi ya Muungano 2026, ambapo Simba SC ilitwaa ubingwa baada ya kuifunga Young Africans SC bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Amaan Complex.
Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha Muungano kupitia sekta tofauti, ikiwemo michezo, ambayo imekuwa daraja muhimu la kuunganisha jamii.
Kwa mujibu wa Mhe. Masauni, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeamua kushiriki moja kwa moja katika uratibu wa ligi hiyo ili kuongeza ubora wa maandalizi pamoja na maslahi ya washiriki na washindi.“Nawapongeza timu zote zilizoshiriki mashindano ya mwaka huu kwani ushiriki wao ndio umeifanya Ligi ya Muungano kuendelea kuwa na mafanikio,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dkt. Riziki Pembe Juma amesema kurejea kwa ligi hiyo kumepokelewa vizuri na wadau wa michezo, hali iliyodhihirisha umuhimu wake kwa jamii.Amesema licha ya kuwepo kwa wasiwasi mwanzoni mwa maandalizi, mafanikio ya msimu huu yameongeza hamasa ya kuanza mapema maandalizi ya msimu ujao.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar, Hussein Ahmada, amepongeza serikali za pande zote mbili kwa kutumia michezo kama nyenzo ya kuimarisha umoja wa Watanzania.
Msimu wa mwaka huu wa Ligi ya Muungano ulihusisha timu nane ambazo ni Simba SC, Young Africans SC, Azam FC na Singida Black Stars kutoka Tanzania Bara, huku Zanzibar ikiwakilishwa na Mlandege FC, KVZ FC, Mafunzo FC na Muembe Makumbi.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni