Serikali imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori, hususan faru weupe ambao ni miongoni mwa spishi zilizo hatarini kutoweka duniani. Hatua hiyo inatekelezwa kupitia Mradi wa Kimkakati wa Uhifadhi wa Faru Weupe unaolenga kuongeza juhudi za uhifadhi, utafiti na elimu kuhusu wanyamapori nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande, wakati wa hafla maalumu ya kuwaachia huru faru weupe 17 katika Eneo la Hifadhi la Ngorongoro. Faru hao ni sehemu ya mradi uliofadhiliwa na Shirika la AndBeyond kwa ushirikiano na Serikali ya Afrika Kusini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Chande alisema mradi huo una manufaa makubwa kwa taifa kwa kuwa unachangia maendeleo ya sekta ya uhifadhi, utafiti na elimu.
“Mradi huu umebuniwa kwa ubunifu mkubwa na una mchango muhimu katika kuongeza utafiti, uhifadhi na utoaji wa elimu kwa jamii. Watu wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani watakuja kujifunza kuhusu faru hawa, wakiwemo wanafunzi na watafiti,” alisema.
Aidha, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuimarisha uhifadhi wa maliasili nchini. Pia aliishukuru Serikali ya Afrika Kusini kwa ushirikiano wake katika kufanikisha mradi huo.Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Alexander Lobora, alisema kuwa kuwaachia huru faru hao kutoka kwenye uzio kutawapa nafasi kubwa zaidi ya kujitafutia malisho huku wakilindwa kupitia mifumo ya kisasa ya ufuatiliaji ndani ya hifadhi.
Alibainisha kuwa Tanzania ipo tayari kupokea faru wengine katika awamu ya pili ya mradi huo kutokana na uzoefu uliopatikana katika awamu ya kwanza.“Lengo kuu la mradi huu ni kuimarisha uhifadhi wa spishi zilizo hatarini kutoweka, sambamba na kutekeleza wajibu wa Tanzania katika mikataba ya kimataifa ya uhifadhi wa wanyamapori,” alisema Dkt. Lobora.
Naye Kamishina wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Abdul-Razaq Badru, alisema taasisi hiyo itaendelea kuimarisha ulinzi wa faru hao kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kuhakikisha wanahifadhiwa kwa manufaa ya taifa na vizazi vijavyo.
Kwa upande wa wadau wa uhifadhi, Mtendaji Mkuu wa Shirika la AndBeyond, Mussa Mathayo, alisema utafiti wa kina ulifanyika kabla ya kuhamishwa kwa faru hao ili kuhakikisha mazingira ya Ngorongoro yanafaa kwa ustawi wao.Aliongeza kuwa shirika hilo lina mpango wa kuongeza idadi ya faru waliobaki ili kufikia faru 36 kama ilivyoainishwa katika makubaliano ya mradi huo.
Umuhimu wa Mradi
Mradi wa uhifadhi wa faru weupe unatarajiwa kuongeza idadi ya wanyama hao nchini, kuimarisha shughuli za utalii wa ikolojia, kuvutia watafiti kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda spishi zilizo hatarini kutoweka.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni