Serikali imeendelea kusisitiza uwajibikaji, ufanisi na thamani ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji na kuimarisha usimamizi wa miradi kwa mfumo wa Washauri Elekezi.
Akizungumza jijini Dodoma, wakati wa kufunga kikao kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli amesema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya Umwagiliaji , ambapo takribani asilimia 30 ya bajeti ya Wizara ya Kilimo inaelekezwa katika miradi ya Umwagiliaji hivyo ni lazima kuona matokeo kwa kuimarisha usimamizi wa miradi hiyo.
Amesisitiza kuwa uwekezaji huo unalenga kuleta mapinduzi ya kilimo kupitia uhakika wa maji na chakula nchini huku akitaka miradi yote kusimamiwa kwa ufanisi ili kuhakikisha “value for money” inapatikana.
Kikao kazi hicho kimehusisha Menejiment ya Tume Wahandisi wa mikoa, Wakandarasi, Washauri Elekezi na wadau wengine akiwemo ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Bodi ya Usajili ya Wakandarasi, Mamlaka ya Mapato, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma na Ofisi ya Hazina.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, amesema Tume imejipanga kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ubora na tija, ambapo mfumo mpya wa usimamizi kupitia washauri elekezi utaongeza ufanisi na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni