Mamlaka za afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo zipo katika hali ya taharuki kufuatia kutoweka kwa msichana mwenye umri wa miaka sita aliyekuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa Ebola baada ya kutekwa kutoka katika kituo cha afya kilichopo mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, watu wenye silaha walivamia kliniki iliyopo karibu na mji wa Butembo katika jimbo la Kivu Kaskazini na kumchukua mtoto huyo pamoja na mama yake. Tukio hilo limeibua hofu kubwa miongoni mwa wataalamu wa afya kutokana na hatari ya kuenea kwa maambukizi ikiwa wagonjwa hao wataendelea kuwa nje ya uangalizi wa kitabibu.
Wataalamu wanaohusika na kudhibiti mlipuko wa Ebola wameonya kuwa kutopatikana kwa mtoto huyo na mama yake kunaweza kuathiri juhudi za kudhibiti ugonjwa huo. Daktari Lubambo Maboko Gaston, ambaye ni meneja wa kukabiliana na mlipuko wa Ebola katika eneo hilo, ametoa wito wa dharura kwa watu hao kujisalimisha au kufikishwa katika kituo cha matibabu haraka iwezekanavyo ili kuendelea kupata huduma stahiki za afya.
Tukio hilo linajiri wakati DR Congo ikiendelea kukabiliana na mlipuko wa Ebola wa aina ya Bundibugyo. Takwimu za Wizara ya Afya kufikia Juni 15 zinaonyesha kuwa jumla ya watu 837 wameambukizwa ugonjwa huo, huku vifo 196 vikithibitishwa. Aidha, watu 49 wameripotiwa kupona na wengine 376 wanaendelea kufuatiliwa kutokana na uwezekano wa kuwa wamekaribiana na wagonjwa.
Maeneo yaliyoathirika zaidi na mlipuko huo ni pamoja na Ituri na Kivu Kaskazini, ambapo mamlaka za afya zinaendelea kuimarisha juhudi za ufuatiliaji wa maambukizi. Timu za wataalamu kutoka Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu zimesema changamoto kubwa inayowakabili ni ugumu wa kuwafuatilia watu waliokaribiana na wagonjwa ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
Hadi kufikia wakati wa kuchapishwa kwa taarifa hii, Serikali ya DR Congo ilikuwa bado haijatoa tamko rasmi kuhusu tukio hilo la utekaji nyara. Hata hivyo, juhudi za kuwatafuta mtoto huyo na mama yake zinaendelea huku mamlaka zikisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wananchi katika kukabiliana na mlipuko wa Ebola na kulinda afya ya jamii.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni