Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limezindua mradi wa vituo vya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme pamoja na Mpango wa Ukopeshaji wa Majiko ya Umeme kwa Wateja (On-Bill Financing – OBF), hatua inayofungua ukurasa mpya wa matumizi ya umeme nchini na kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya nishati safi.
Akizindua miradi hiyo Juni 11,2026, jijini Dodoma, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Tanzania kushiriki kikamilifu katika mageuzi ya matumizi ya nishati safi duniani huku ikilenga kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi.
Amesema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati, hali iliyowezesha uzalishaji wa umeme nchini kufikia zaidi ya megawati 4,000 na kuweka msingi wa matumizi mapana ya umeme katika sekta mbalimbali za uchumi.
Katika kuimarisha matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme, TANESCO kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) imepokea mashine 50 za kisasa za kuchajia vyombo hivyo kutoka kampuni ya AUTEL ya China. Mashine hizo zitafungwa katika maeneo mbalimbali ya kimkakati nchini ili kurahisisha huduma za uchaji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema Shirika limejipanga kuongoza mageuzi ya matumizi ya umeme nchini kwa kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme wa kutosha.
Uzinduzi wa miradi hiyo unaashiria hatua mpya ya kupanua matumizi ya umeme nchini kutoka matumizi ya kawaida ya majumbani hadi sekta za usafiri, kupikia na shughuli za uzalishaji mali, sambamba na juhudi za Taifa kuelekea uchumi wa kijani na maendeleo endelevu.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni