Breaking


Jumatano, 3 Juni 2026

TANZANIA NA DENMARK KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA AFYA NA KUDHIBITI MAGONJWA YA MLIPUKO


Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, amekutana na ujumbe wa wataalamu kutoka Denmark kwa lengo la kujadili na kuimarisha maeneo mbalimbali ya ushirikiano katika sekta ya afya kati ya Tanzania na nchi hiyo ya Ulaya.

Ujumbe huo ulijumuisha wawakilishi kutoka Ubalozi wa Denmark, Wizara ya Mambo ya Ndani na Afya ya Denmark, pamoja na wataalamu kutoka taasisi zinazojihusisha na udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza.

Mazungumzo hayo yalifanyika Juni 2, 2026, jijini Dodoma, yakijikita katika masuala muhimu ya afya ya umma, ikiwemo kukabiliana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa, kuimarisha mifumo ya ugunduzi na uchunguzi wa magonjwa, pamoja na kuboresha mwitikio wa haraka wakati wa milipuko ya magonjwa.

Aidha, pande hizo mbili zilijadili matumizi ya teknolojia za kisasa katika kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa afya kwa umma, hatua inayolenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya na kudhibiti changamoto zinazoweza kujitokeza katika jamii.

Katika kikao hicho, Tanzania na Denmark pia zilizungumzia fursa za ushirikiano wakati Tanzania ikiwa katika hatua za kuanzisha Taasisi ya Taifa ya Afya kwa Umma. Serikali ya Denmark imeahidi kushirikiana na Tanzania kwa kubadilishana uzoefu na utaalamu katika kuanzisha na kuendesha taasisi hiyo.

Taasisi ya Taifa ya Afya kwa Umma inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha tafiti za afya, mifumo ya taarifa za afya, utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, pamoja na matumizi ya taaluma za microbiolojia, epidemiolojia na bioinformatiki katika kuboresha afua za afya kwa wananchi.


Akizungumza wakati wa mkutano huo, Dkt. Shekalaghe amepongeza ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Denmark ambao umeendelea kwa zaidi ya miaka 61. Amesema ushirikiano huo umeleta manufaa makubwa katika sekta mbalimbali, hususan afya, na kuahidi kuendeleza juhudi za kuibua maeneo mapya ya ushirikiano yenye manufaa kwa pande zote mbili.


Ushirikiano huo unaendelea kuunga mkono dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kujenga mfumo imara wa afya wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za afya ya umma kwa ufanisi, huku ukiimarisha usalama wa afya kwa wananchi na maendeleo ya sekta ya afya nchini.


Hakuna maoni: