Na Beda Msimbe TBN Moscow.
Tanzania na Urusi zipo katika hatua za mwisho za majadiliano za matumizi ya fedha za malipo kwa lengo la kuimarisha biashara baina yao.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo kwenye mahojiano na waandishi wa habari waliopo katika msafara wa ziara ya kitaifa ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Urusi.
Alisema mataifa hayo mawili yatasaini hati za makubaliano kabla kumalizika kwa ziara.
Alisema kuna urari wa biashara wa Dola za Marekani milioni 200 hivyo hatua hiyo ya kufikia makubaliano itafungua njia ya ushirikiano kwenye ufanisi katika masuala ya uwekezaji na biashara.
Alifafanua kuwa makubaliano hayo yatahusisha matumizi ya shilingi ya kitanzania.
Alisema Urusi ambayo ikishiriki katika ukombozi wa kisiasa sasa inakuja kusaidia ukombozi wa kiuchumi na iko mbele katika kilimo uchakataji na uzalishaji, mbegu bora, madini itakuwa msaada mkubwa katika utekelezaji dira ya maendeleo 2025 ambayo itaanza kitumika Julai mwaka huu. Profesa Mkumbo alisema kuna manufaa makubwa katika ziara hiyo ni kuwezesha Ujenzi wa Reli ya Kusini kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Aidha alisema ili kurahisisha mawasiliano katika utalii, Tanzania na Urusi zipo katika hatua ya mwisho ya kuingia makubaliano yatakayowezesha Shirika la Ndege la Tanzania kufanya safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Moscow.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni